Home BIASHARA Tanzania, Oman zasaini mkataba kuondoa kodi mara mbili

Tanzania, Oman zasaini mkataba kuondoa kodi mara mbili

0 comment 9 views

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Kisultan ya Oman, zimetia saini Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi.

Mkataba huo unajulikana Kaman Agreement for the Elimination of Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax Avoidance and Evasion.

Mkataba huo umesainiwa Mjini Mascut nchini Oman na Waziri wa Fedha wa Tanzania,  Dkt. Mwigulu Nchemba na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman Nasser Al-Jashmi.

Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba akiwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Nasser Al-Jashmi.

Ameongeza kuwa Mkataba huo utawezesha wawekezaji na wafanyabiashara wanaofanya shughuli kati ya Tanzania na Oman kutozwa kodi mara moja pekee, badala ya kutozwa mara mbili kwa mapato ya aina moja, hali ambayo awali ilikuwa ikikwaza ustawi wa biashara kwa pande zote mbili.

Mkataba huo pia unalenga kuvutia mitaji mikubwa kutoka Oman kuja kuwekeza Tanzania, hususan kupitia kampuni kubwa zinazomilikiwa na familia za kifalme, sambamba na wawekezaji binafsi ambapo kupitia uwekezaji huo, Tanzania inatarajia kunufaika na ukuaji wa sekta za uzalishaji, maendeleo ya viwanda, na kuongezeka kwa ajira kwa wananchi.

Dkt. Nchemba amesema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni hatua muhimu katika jitihada za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, za kufungua uchumi wa nchi kwa kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

“Aidha, wawekezaji wa Kitanzania sasa wataweza kuwekeza Oman bila vizuizi vya kikodi, huku wakilindwa na mkataba huo ili kuepusha kulipishwa kodi mara mbili.

Hatua hiyo pia inatoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kupanua shughuli zao katika masoko ya kimataifa, hasa katika ukanda wa Ghuba,” ameeleza Waziri Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba amesema kuwa mkataba huo unatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Oman, huku Oman ikivutiwa zaidi na fursa za uwekezaji nchini Tanzania kutokana na jiografia yake ya kimkakati, vivutio vyake vya kiuchumi, na mazingira bora ya uwekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter