Kampuni ya simu za mkononi inayoongoza nchini, Vodacom Tanzania, leo imetangaza kuunga mkono jitihada za kuboresha afya zinazofanywa na Wizara ya Afya ya Zanzibar na kampuni ya Norvatis kutoka nchini Uswisi kufanikisha kuondoa changamoto kubwa ya uhaba wa madawa kisiwani Zanzibar.
Uhaba wa madawa hujitokeza wakati ambapo maduka ya dawa hushindwa kuwa na dawa za kutosha kulingana na mahitaji. Hali hii husababisha madhara makubwa katika kutoa huduma za afya. Mfumo huu mpya utawezesha ufuatiliaji wa karibu wa akiba ya dawa zilizopo na kupunguza uwezekano wa kutokea uhaba wa dawa.
Utekelezaji wa mfumo huu mpya wa kufuatilia ugavi wa madawa kupitia programu ya ujumbe wa simu za mkononi inayojulikana kama SMS kwa Maisha (SMS for life), Wizara ya Afya inalenga kuboresha upatikanaji wa dawa muhimu kwa watu wa Zanzibar na pia kuwezesha huduma nzuri za afya na ustawi kwa watu wanaoishi Zanzibar. Vodacom na Novartis zitashirikiana kwa kutumia teknolojia iliyozinduliwa na kampuni tanzu ya Vodafone (Mezzanine) na kutoa mafunzo kuhakikisha Zanzibar inanufaika kupitia mapinduzi ya kidigitali.
“Kliniki zilizopo Zanzibar mara nyingi zimekuwa na changamoto ya kufanikisha upatikanaji wa madawa muhimu. Programu hii mpya itafanikisha kukabiliana na changamoto hii kupitia ubunifu wa teknolojia ambao utasaidia taasisi zinazotoa huduma za afya kufuatilia mahitaji na mfumo wa ugavi wa madawa, ukianza kutumika Zanzibar, utaboresha zaidi mfumo wetu wa utoaji wa huduma za afya, kuhudumia vizuri wagonjwa na kuboresha maisha” alisema Harusi Said Suleiman wa Wizara ya Afya ya Zanzibar.
Programu ya ujumbe wa simu za mkononi inayojulikana kama SMS kwa Maisha, hutumia simu za mkononi kupitia teknolojia inayojulikana kitaalamu kama Cloud kuwezesha kufuatilia usambazaji wa madawa. Teknolojia hii itatumika katika vituo vya afya vilivyopo chini ya serikali vipatavyo 190 Zanzibar (Pemba na Unguja), kuwezesha kupata taarifa ya kila wiki ya mahitaji na matumizi ya dawa. Kwa kufanya hivyo, itasaidia kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana kwa wakati katika vituo hivi kulingana na mahitaji ya wagonjwa wanaowahudumia.
Nathan Mulure, Mkuu wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika inayosimamia Biashara ya bidhaa za Kijamii ya Novartis, amesema makubaliano haya ya kufanya kazi pamoja ni mfano mzuri wa sekta za umma na za kibinafsi kushirikiana katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya huduma za afya. “Kuwezesha Wizara ya Afya kuboresha mfumo wa huduma za afya nchini Tanzania, kupitia mradi kama huu wa SMS kwa Maisha ni moja ya dira yetu ya kuboresha huduma za afya barani Afrika. Kwa ushirikiano wa pamoja na Vodacom na Mezzanine, tunaweza kuleta mabadiliko chanya kupitia ubunifu wa teknolojia kuhakikisha mfumo wa huduma za afya wa Zanzibar unakidhi matakwa ya wagonjwa wanaohitaji huduma za kiafya”alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara za makampuni wa Vodacom, Arjun Dhillon alisema “Ubunifu unaolenga kutatua changamoto za kiafya ni moja ya eneo ambalo kampuni ya Vodacom Tanzania tunalipa kipaumbele kikubwa. Tunayo furaha kushirikiana na kampuni ya Mezzanine kufanikisha ubunifu wa kiteknolojia katika kuboresha huduma za afya kwa watu wa Zanzibar. Kupitia SMS kwa Maisha vituo vya afya vilivyopo maeneo ya mbali na mjini vitaweza kutoa taarifa ya mahitaji yake ya madawa kwa haraka na kwa ufanisi.”