Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi, wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo ametoa wito kwa wakazi wa kijiji cha Kigombe wilayani Muheza mkoani Tanga kuacha kushiriki kwenye biashara za magendo na badala yake, watumie maeneo yaliyo rasmi na yaliyoidhinishwa kisheria kwa ajili ya upitishaji wa bidhaa.
Kayombo amesema hayo wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa ndani uliofanyika eneo la sokoni, akiwa ameambatana na viongozi kadhaa kutoka TRA mkoa wa Tanga. Mkurugenzi huyo amewatahadharisha wananchi wa eneo hilo kuacha kutumia njia zisizo rasmi kusafirisha bidhaa zao na badala yake watumie bandari ya Pangani ambayo ipo kisheria kwani wasipofanya hivyo wanaweza kuwajibishwa na vyombo vya sheria.