Home BIASHARA Umuhimu wa Barcode katika kupata masoko zaidi

Umuhimu wa Barcode katika kupata masoko zaidi

0 comment 193 views

Teknolojia ya barcode(Msimbomilia) imekuwa ni msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa hasa katika suala zima la kusimamia mahesabu, upataji wa masoko ya nje na ndani, kujua idadi ya bidhaa zilizopo nk. Pia kupitia teknolojia hii tasnia ya biashara imeendelea kukua ulimwenguni ambapo bidhaa mbalimbali zimekuwa zikizunguka kila pande ya dunia hali iliyopelekea uchumi kuendelea kukua duniani.

Kwa Tanzania, watu wengi wamezoea kuona matumizi ya msimbomilia katika maduka makubwa maarufu kama ‘supermarkets’, na mabasi ya mwendokasi lakini ieleweke kuwa msimbomilia hutumika katika bidhaa na huduma mbalimbali . Pia maboresho ya teknolojia yanaruhusu usomaji wa msimbomilia hata kwa simu janja si lazima mtu awe na kifaa maalum cha kusomea.

Ndio maana serikali imekuwa ikiwasisitiza wafanyabiashara nchini kutumia namba ya utambulisho wa bidhaa zinazozalishwa Tanzania na kampuni iitwayo GS1 ili kuweza kupata masoko ya ndani na nje.  Kampuni hiyo inapatikana katika mtandao wa intaneti ikiwa mfanyabiashara anataka kujisajili mtandaoni  au kujua mchakato mzima wa msimbomilia (https://www.gs1.org/). Msimbomilia unaowakilisha Tanzania ni  620 (BARCODE 620).

Faida za kutumia msimbomilia

  • Msimbomilia husaidia katika utunzaji wa kumbukumbu ya bidhaa husika hasa kama bidhaa hizo zinazalishwa kwa wingi. Pia kwa upande wa wafanyabiashara wakubwa msimbomilia husaidia kupata taarifa za haraka kuhusu bidhaa hii huepusha upotevu wa muda katika kujua bidhaa zilizouzika, kiasi cha mzingo uliobakia, nchi au mahali bidhaa husika zinakozalishwa nk. Hivyo kupitia kompyuta kifaa kinachotumika kusoma msimbomilia kitatoa taarifa kamili kuhusu bidhaa husika mara tuu kifaa hiko kitakapopitishwa katika nembo ya msimbomilia.
  • Ni dhahiri kuwa nembo za msimbomilia huwekwa katika bidhaa ambazo zipo tayari kwa matumizi na si malighafi. Hivyo kama kila mfanyabiashara au mjasiriamali atahamasika kupata nembo ya msimbomilia basi itakuwa rahisi kwa wafanyabiashara nchini kutengeneza bidhaa ambazo ziko tayari kuingia sokoni. Hivyo kutangaza bidhaa ndani na nje ya nchi na kukuza uchumi binafsi na hata wa nchi kwa ujumla kwani kuna utofauti mkubwa wa bei kati ya mtu anaeuza malighafi na Yule anayeuza bidhaa ambayo iko tayari.
  • Si rahisi kufanya makosa ya kimahesabu ikiwa mfanyabiashara anatumia nembo ya msimbomilia katika bidhaa zake. Hii huepusha upotevu wa fedha kwa asilimia kubwa kwani ikiwa wafanyakazi watafanya mahesabu kikawaida wanaweza kufanya makosa ya kibinadamu na kukosea kuingiza baadhi ya taarifa.
  • Katika suala la huduma kwa wateja, kama bidhaa zina msimbomilia na kuna wateja wengi basi nembo hiyo huepusha msongamano na kuepuka kumpotezea mteja muda wake. Kutokana na hilo mfanyabiashara anaweza kupata wateja zaidi hasa wa kudumu kutokana na uharaka wa utoaji huduma.
  • Msimbomilia humrahisishia mfanyabiashara kujua mauzo aliyoyafanya kwa siku, wiki, mwezi na hata mwaka. Hivyo baada ya kutumia muda mrefu kufanya mahesabu, mfanyabiashara hutumia muda mfupi kutokana na taarifa zilizorekodiwa katika kompyuta kupitia usomaji wa bidhaa zilizouzwa na zile zilizobakia.

Mbali na hayo, kuna muda huwa kunakuwa na punguzo la bei na inaweza kutokea kuwa wahusika katika biashara hawajafanya mabadiliko katika mfumo wa kusomea nembo za msimbomilia, hali hiyo inaweza kuleta mkanganyiko baina ya wauzaji na wateja na hata upotevu wa muda wakati mabadiliko yanafanyiwa kazi. Hivyo ni muhimu kwa wamiliki wa biashara/wafanyakazi kuwa makini na mabadiliko yoyote yanayotokea ili kuendelea kutoa huduma kwa wateja.

Pia si kila mfanyabiashara au mjasiriamali ana uelewa wa matumizi ya nembo hizi hivyo elimu kwa wafanyabiashara inatakiwa kutolewa zaidi katika makundi, na hata ana kwa ana na kampuni inayotoa nembo hizi.

Aidha, vifaa vya kusomea nembo hizi huhitaji fedha ili kuweza kuvinunua, na hata usajili wa nembo hizi huhitaji kiasi cha fedha ili kuweza kukamilika. Kwakua asilimia kubwa ya wafanyabiashara nchini bado ni wadogo, basi serikali au taasisi zisizo za kiserikali zingeweka utaratibu ambao utawasidia wafanyabiashara hasa wadogo na wa kati( wanaotengeneza bidhaa zenye ubora stahiki) kupata vifaa na kujisajili kwa bei rafiki ili kuweza kutangaza biashara zao katika masoko makubwa zaidi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter