Home BIASHARA Umuhimu wa kumbukumbu za kifedha

Umuhimu wa kumbukumbu za kifedha

0 comment 208 views

Ni jambo la kawaida kusikia mtu leo ana fedha na kesho hana. Hivyo hata katika biashara, ni muhimu sana kutunza kumbukumbu za kifedha ili kujua muelekeo wa biashara yako. Wahenga walisema ‘Mali bila daftari huisha bila habari’ kutokana na msemo huo tu mfanyabiashara anatakiwa kujua ni jinsi gani kumbukumbu ni muhimu ili mambo yaende na matunda yaonekane.

Unapokuwa na kumbukumbu kuhusu mapato na matumizi katika biashara ni rahisi kufanya maamuzi na kujua hatua zipi uchukue ili kuleta maendeleo zaidi.

Faida za kuweka kumbukumbu:

Kuweka kumbukumbu za kifedha husaidia kujua taarifa fupi ya biashara, kunamsaidia mfanyabiashara kujua hali ya kifedha kwa ujumla kwa mfano kujua faida, hasara katika biashara, mali, madeni n.k. hivyo kuleta urahisi kwa mfanyabiashara katika kufanya maamuzi.

Ikiwa mmiliki wa biashara amemuajiri mtu inakuwa rahisi kwa mmiliki kumuamini mfanyakazi wake kupitia kumbukumbu. Pia mfanyakazi hufanya kazi kwa bidii na katika hali ya uaminifu ili asipoteze kazi yake.

Kuweka kumbukumbu hurahisisha kupanga mipango ya baadae. Kutokuweka kumbukumbu kunaweza kusababisha biashara isiendelee, kupata hasara nyingi  na kupelekea mtaji kutokua hivyo kuwa ngumu kutimiza malengo ya baadae.

Vilevile kwa kutunza kumbukumbu mfanyabiashara anakuwa huru katika maswala ya kisheria, kwa mfano ni kawaida kwa Mamlaka ya Kodi nchini  (TRA) kupitia vitabu vya kumbukumbu vya wafanyabiashara ili kujua kama wanalipa kodi stahiki, sasa kutokuwa na kumbukumbu kunaweza kusababisha matatizo makubwa katika biashara na kuharibu jina la biashara kwa ujumla.

Kwa ujumla kuna mifumo miwili ya kuweka kumbukumbu za kifedha katika biashara mifumo hiyo ni: Kurekodi kwa kuzingatia miamala ya fedha taslimu (huu si lazima mfanyabiashara awe na ujuzi) na mfumo wa kurekodi kwa kuzingatia msingi wa muamala,madeni, hali ya fedha (huu ni mfumo rasmi ambao huelezea mapato,matumizi, madeni, hasara na hali ya biashara)

Hivyo ni muhimu kuchagua mfumo ambao unaendana na biashara au shughuli yako ili kujua maendeleo ya biashara yako na kwenda sawa na sheria na kanuni za biashara.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter