Mgahawa ni moja kati ya biashara zinazolipa hapa nchini. Kutokana na hilo, hakuna urahisi katika biashara hii kuanzia kwa mmiliki hadi wafanyakazi. Na ili watu wapende kula katika mgahawa wako unatakiwa kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa ikiwa ni pamoja na usafi, muonekano wa mgahawa wako n.k.
Kama umeamua kufanya biashara hii zingatia haya:
- Si kila mtu lazima awe mmiliki wa mgahawa
Unapenda kupika? Vizuri, unapenda kula? Vizuri zaidi, unapenda kuburudisha? Jambo zuri lakini hayo yote hayawezi kukufanya uwe na vigezo vya kumiliki mgahawa. Mambo unayotakiwa kuzingatia ni pamoja na je unapenda kufanya kazi masaa mengi? Unaweza kumudu kutolipwa kwa muda? Unaweza kununua bima ya afya? Na sio kufikiria tu kufungua biashara. Wazo la kuwa bosi ni zuri lakini linakuja na majukumu mengi kuliko unavyoweza kufikiria.
- Eneo
Kati ya vitu muhimu kwenye biashara hii ni eneo. Hutakiwi kupuuzia swala hili kwasababu eneo likiwa zuri uhakika wa kupata wateja wengi ni mkubwa na kufungua mgahawa eneo baya kutakwamisha ndoto zako za kuwa na mgahawa kwa muda mrefu. Hivyo kama una wazo la eneo ambalo unaweza kufungua mgahawa wako fanya utafiti na kuwa tayari kuuanzisha mgahawa katika eneo tofauti.
- Hakuna mgahawa wa bei rahisi
Inategemea na ukubwa, mandhari ya mgahawa wako mpya unatakiwa kujua kuwa biashara ya mgahawa haianzishwi kwa fedha ndogo. Unatakiwa kujipanga na kuhakikisha una fedha za kutosha kwa ajili ya uanzilishi wa mgahawa wako. Hivyo unatakiwa kuandika kila kitu kinachohitaji fedha na kuandika pembeni kama unaweza kumudu gharama za mambo yote kwa kiasi gani ili uweze kufanya maamuzi sahihi.
- Dhana (concept) ya mgahawa ni muhimu
Dhana ya mgahawa itakuongoza katika mambo mengi ya mgahawa wako ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa orodha ya vyakula na bei (menu), muonekano wa mgahawa, na jina la mgahawa. Kila muanzilishi wa mgahawa siku zote hutaka mgahawa wake kuwa wa kipekee na bora zaidi kuliko migahawa mingine. Hivyo usichanganye mambo sababu utawapa wateja wako wakati mgumu na kuwafanya kwenda sehemu nyingine.
- Mpango wa biashara
Kwa sababu biashara ya mgahawa mzuri inahitaji mtaji mkubwa, hivyo ni muhimu kuwa na mpango wa biashara ikitokea utahitaji wawekezaji wa nje kuja kuwekeza katika mgahawa wako. Aidha, mpango wa biashara ni muhimu kwa mtu ambaye anamiliki biashara kwa mara ya kwanza kwa kuwa itamsaidia kujua muelekeo wa biashara yake.