Home BIASHARA Unataka kukua kibiashara 2020? Soma hii

Unataka kukua kibiashara 2020? Soma hii

0 comment 137 views

Ni dhahiri kuwa kila biashara hupitia changamoto za aina yake. Mbinu za kutatua changamoto hizo hupelekea biashara kukua au kutokusonga mbele, hivyo kila mfanyabiashara ana jukumu kubwa la kuchukua hatua sahihi pindi changamoto zinapokuwa zimejitokeza. Inaelezwa kuwa ni 80% tu ya biashara mpya hufikia mwaka na nusu ya asilimia hiyo husherekea miaka mitano ya uwepo wa biashara hizo katika tasnia mbalimbali. Hivyo ikiwa unataka kukua zaidi kibiashara na kuwavutia wateja wapya mwakani na hata miaka inayokuja ni muhimu kuzingatia haya:

Wahimize wateja kutoa maoni na ushuhuda kuhusu biashara yako, tupo katika zama za kidijitali mtandao wa intaneti unatumika kwa kiasi kikubwa katika tasnia ya biashara. Wateja hasa wale wapya hupendelea kuona watu wengine wanafikiriaje kuhusu bidhaa au huduma ambayo wanataka kulipia. Pia ripoti ya hivi karibuni inaeleza kuwa 92% ya wateja husita kufanya manunuzi ikiwa hakuna ushuhuda au maoni kuhusu bidhaa au huduma husika. Hivyo kama unatumia tovuti, mitandao ya kijamii, blogu nk kutangaza biashara yako jitahidi kuwahamasisa wateja wako kutoa maoni yao baada ya kufanya manunuzi kwamfano unaweza kutoa zawadi kwa watu ambao wanatoa mirejesho au  punguzo la bei ikiwa watakuja tena kufanya manunuzi na kutoa mrejesho wa bidhaa au huduma husika, kwa kufanya hivyo unakuwa unawahamasisha wateja wapya na wa zamani.

Rahisisha ufanisi wa kazi kwa wafanyakazi wako, biashara nyingi zilizofanikiwa zimejenga utamaduni ambao unawarahisishia wafanyakazi kufanya kazi zao huku wakipata muda wa kujihusisha na masuala binafsi. Kwamfano Microsoft Japan imefanya utafiti mwaka huu na kugundua kuwa mauzo yaliongezeka wa 40% wakati wa majaribio  ambayo wafanyakazi walitakiwa kufanya kazi siku nne tu kwa wiki. Hivyo kulingana na biashara yako, jaribu kutengeneza mbinu ambazo zitawafanya wafanyakazi waone urahisi wa kufanya kazi zao hii itawahamasisha kufanya kazi kwa bidii zaidi na kuweza kufanya mambo binafsi. Kwa mfano ikiwa wafanyakazi wanaweza kufanya kazi  zao bila kufika ofisini basi unaweza kuwapa chaguo la kufika kazini siku tatu huku wakiendelea kufanya kazi siku mbili majumbani kwao.

Mifumo ya kisasa ya ulipaji, kadri siku zinavyozidi kwenda mifumo mipya ya ulipaji wa bidhaa na huduma inaendelea kuanzishwa. Ieleweke kuwa moja ya mambo ambayo huvutia wateja kufanya manunuzi zaidi ni namna ya kufanya malipo. Hivyo kulingana na biashara yako mbali na kukubali fedha taslimu unaweza kuwekeza katika mifumo mipya ya ulipaji wa bidhaa ili kurahisisha mchakato mzima wa biashara na wateja wako. Mbali na kulipa na mitandao ya simu kama mpesa, tigopesa, halopesa, tpesa nk unaweza kuanzisha mfumo wa kulipa kwa kadi, na kuna baadhi ya biashara duniani zimeshaanza kukubali malipo kutokana na cryptocurrencies kama bitcoin nk hivyo jiandae kufanya biashara kisasa, na kwa usalama zaidi.

‘Get social’, mitandao ya kijamii imeleta mafanikio makubwa kwa biashara nyingi hasa ambazo hazina uwezo wa kutangaza biashara katika televisheni, redio, na hata magazeti. Hivyo mbali na kuuza bidhaa au huduma katika mitandao hii wamiliki wa biashara wanapaswa kutoa elimu kuhusu tasnia husika kulingana na uzoefu nautaalamu walio nao, kueleza maono ya biashara zao, kujihusisha na masuala ya msingi katika jamii na kutangaza katika majukwaa hayo ili kuweza kuhamasisha watu wengine kufanya mambo ambayo yanalenga kujenga uchumi na tasnia mbalimbali. Lengo ni kuhakikisha wateja wanafikiria brandi yako kila wakiwa wanataka kufanya manunuzi.

Hudhuria  au andaa hafla za kibiashara, siku hizi kuna hafla mbalimbali za kibiashara ambazo huandaliwa na makampuni maalum na hata wamiliki wa biashara mbalimbali. Hivyo fatilia hasa katika mitandao ya kijamii kuhusu hafla zinazoandaliwa na makampuni ambayo yapo katika Tasnia unayojihusisha nayo kisha hudhuria ili kuweza kukuza mtandao na hata kuwajulisha watu wengine kuhusu uwepo wa biashara yako na malengo yake. Aidha unaweza kushirikiana na kampuni nyingine ambayo inaendana na kampuni yako na kuandaa hafla ambayo itawakutanisha manguli-wataalamu, wateja na hata wawekezaji; kwa kufanya hivyo unakuwa umejitangaza na kupanua wigo katika biashara yako.

Mbali na hayo, jambo la msingi ambalo kila mfanyabiashara anapaswa kufanya ni kumsikiliza kila mteja. Kwa kufanya hivyo inakuwa rahisi kujua mambo gani yanatakiwa kufanyiwa marekebisho au kuboreshwa, pia kwa kuwasikiliza wateja mfanyabiashara anapata nafasi ya kujifunza na kujua matakwa ya wateja hali itakayopelekea biashara kukua.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter