Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi amewataka watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kuacha kuizungumzia vibaya nchi yao na badala yake kuisaidia serikali kutafuta wawekezaji ili waje kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo iliyopo nchini.
Prof. Kabudi amesema ili kuifikisha nchi katika uchumi wa kati, ushirikiano wa ndani na nje ya nchi ni muhimu na kutoa wito kwa watanzania hao kushirikiana na serikali ili kuwavutia wawekezaji kuja nchini na sio kuwakimbiza. Pia amesema kuwa serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), njia bora zimewekwa ili kumsaidia muwekezaji anapokuja nchini.
“Ninachowahakishia watanzania mnaoishi nje ya nchi kuwa nyumbani ni pazuri na kuna fursa nyingi tena zinazoweza kuwanufaisha nyie mnaoishi nje ya nchi, kikubwa ninachowaomba mfanye ni kuitangaza Tanzania vema nje ya nchi ili wawekezaji waje. Sasa mimi ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mambo ya Nje nilikuwa Waziri wa Sheria na Katiba, nilikuwa na jukumu la kuimarisha mifumo mizuri ya Sheria nchini ambapo ni kazi nimefanya kiufanisi, sasa nawahakikishia kama Waziri wa Mambo ya Nje mje nyumbani mambo ni salama na shwari”. Ameeleza Waziri huyo.