Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amesema utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta kutoka (Hoima) Uganda hadi Tanga haujasimama na kueleza kuwa, hatua za utekelezaji wa mradi huo bado zinaendelea. Dk. Kalemani amesema hayo jijini Dar es salaam katika mkutano uliokuwa ukijadili utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa bomba hilo uliomkutanisha Waziri huyo na Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni.
Dk. Kalemani amefafanua kuwa, utekelezaji wa mradi huo upo katika hatua nzuri na kudai pande zote mbili zimejadiliana na kukubaliana kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa pamoja na hatua za utkelezaji za mradi.
“Mradi haujasimama tunaendelea na utekelezaji tumekubaliana tukamilishe ndani ya wakati tuliokubaliana pande zote mbili”. Amesema Dkt. Kalemani.
Katika maelezo yake, Waziri Kalemani amesema upande wa Tanzania tayari wamekamilisha tafiti ya tathmini ya mazingira, ustawi wa jamii pamoja ulipaji fidia kwa wananchi mkoani Tanga.
Naye Waziri Muloni wa Uganda amesema watahakikisha watafikia makubaliano na makampuni ili kufanikisha kusaini utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kumalizika mwaka 2020. Waziri huyo Amefafanua kuwa ifikapo Januari 2019, mkutano mwingine utafanyika nchini Uganda na masuala yaliyobaki yatajadiliwa ili makampuni yaanze utekelezaji mara moja.