Home BIASHARAUWEKEZAJI Faida ya mali zisizohamishika

Faida ya mali zisizohamishika

0 comment 87 views

Kila aina ya uwekezaji huwa ina faida na hasara. Lakini inaelezwa kuwa mamilioni ya watu wanakubali kuwa uwekezaji katika mali isiyohamishika maarufu kama ‘Real Estate’  una faida zaidi kuliko hasara.

Hivyo ikiwa unataka kufanya uwekezaji zaidi na kukuza uchumi wako, ni muhimu kujua faida unazoweza kupata ikiwa utawekeza katika mali zisizohamishika.

Baadhi ya faida hizo ni kama zifuatavyo:

Chaguzi tofauti

Uwekezaji katika mali zisizohamishika huleta fursa mbalimbali zisizoisha, hivyo ni rahisi kufanya uchaguzi tofauti tofauti. Kwamfano unaweza kuwekeza katika makazi,maeneo kwaajili ya biashara, maeneo kwaajili ya viwanda,mali za kukodisha,vyumba, nyumba za familia, kwa mkakati tofauti tofauti ya kukodisha (kodi za muda mfupi na muda mrefu) nk. Hivyo haijarishi kiasi cha fedha ulicho nacho uwekezaji katika mali zisizohamishika ni suluhisho sahihi katika mahitaji na matarajio yako kwani kwa namna moja au nyingine faida lazima ipatikane.

Maarifa

Si lazima uwe na utaalamu au ujuzi ili kuweza kuwekeza katika mali isiyohamishika. Mbali na hilo kuna vyanzo mbalimbali vya mtandao na vitabu ambavyo vinaweza kukuongoza ikiwa unataka kufanya uwekezaji katika mali zisizohamishika. Hivyo ni rahisi kuwekeza na kupata ujuzi kadri siku zinavyokwenda katika mali isiyohamishika ukilinganisha na aina nyingine za uwekezaji.

Uwekezaji wa ziada

Ni rahisi kufanya uwekezaji huu ikiwa unafanya kazi, hivyo unaweza kuendelea na kazi yako huku ukiwekeza katika mali isiyohamishika. Hii husaidia hasa kwa wawekezaji wa mwanzo kufanya kazi na kupata rasilimali za kifedha ili kuboresha uwekezaji huo na kuhakikisha mahitaji mengine yanapatikana. Pia baada ya uwekezaji huu kuanza kuleta faida muwekezaji anaweza kuendelea au kuacha kazi.

Mali inayoonekana

Watu wengi hupenda kuwa na uhakika na jambo wanalotaka kuwekeza. Hivyo watu wengi huchukulia uwekezaji huo kuwa sio wa kuogopesha ikilinganishwa na uwekezaji katika hisa au uwekezaji aina nyingine ambao hauonekani.

Hatari ndogo

Moja ya viashiria ambavyo wawekezaji wengi hutazama wakati wa kuamua wapi kuwekeza ni hatari. Mali isiyohamishika siku zote huwa na hatari ndogo kwa sababu kwanza unakuwa umewekeza katika mali inayoonekana, bima inaweza kukuokoa ikiwa tatizo litatokea, kwa ujumla huwezi kupoteza fedha zako zote hata kama kutatokea mfumuko wa bei na una uwezo wa kuongeza kodi kulingana na kuongezeka kwa kiwango cha bei. Hivyo kama muwekezaji huwezi kupoteza fedha.

Mapato yanayoendelea

Lengo la kuwekeza ni kujipatia fedha na kuleta maendeleo zaidi hivyo kwa kununua mali isiyohamishika unaweza kuanza kujipatia fedha moja kwa moja ili mradi tu upate wapangaji ambao kulingana na makubaliano malipo yataendelea kutolewa na wapangaji hao kwa mfano inaweza kuwa kwa mwezi, miezi sita au kila mwaka.

Katika uwekezaji wa aina hii ni rahisi kujipatia faida za muda mrefu kwa sababu bei uliyonunulia lazima ibadilike hivyo baada ya miaka kadhaa mbeleni unaweza kuuza mali hiyo kwa fedha nyingi zaidi. Ni muhimu kujua faida na hasara za uwekezaji huu na kufanya utafiti kuhusu eneo unalotaka kununua mali hiyo ili kufanya maamuzi sahihi.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter