Naibu Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya mtandao wa simu wa Halotel Nguyen Van Son amesema kampuni hiyo imepanga kuwekeza takribani Dola milioni 700 za Marekani katika sekta ya mawasiliano hapa nchini. Van Son amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa, uwekezaji huo utaiwezesha Halotel kuwafikia wateja zaidi ya milioni sita kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Van Son amewaambia waandishi wa habari kuwa Halotel inalenga kuboresha huduma zake katika kipengele cha fedha kwa njia ya mtandao (Halopesa) pamoja na kitengo cha teknolojia ya mawasiliano (ICT) kwa ajili ya wateja kutoka mashirika binafsi pamoja na serikali.
Mbali na hayo, Naibu huyo ameeleza kuwa kampuni hiyo inapoadhimisha miaka mitatu, tayari imefanikiwa kufanya uwekezaji wa Dola milioni 500 za Marekani na ikiwa ni kampuni inayoongoza katika uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano inayofikia asilimia 95 ya wananchi wote, huku ikiwa na vituo vya kupokea mawasiliano 4,400 kwa umbali wa kilomita 18,300.
“Halotel imelenga kuwafikia watu walioko pembezoni mwa miji kwa kuwapa gharama nafuu za mawasiliano huku ikiwa tayari imewafikia wananchi zaidi ya milioni tatu sambamba na milioni moja wengine waliojiunga na mtandao wa Halopesa”. Amesema Van Son.