Home VIWANDAUZALISHAJI Dk. Tizeba: Tanzania yajitosheleza kwa chakula miaka mitano mfululizo

Dk. Tizeba: Tanzania yajitosheleza kwa chakula miaka mitano mfululizo

0 comment 35 views

Na Mathias Canal-WK, Tunduma-Songwe

Tanzania imeendelea kuwa ghala la chakula kwa nchi za jirani kwa kipindi kirefu baada ya kujitosheleza kwa chakula takribani kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.

Tanzania imeweza kuuza ziada ya mazao mbalimbali ya chakula katika nchi za nje. Kulingana na takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kipindi cha mwezi Juni 2017 hadi Juni 2018 yameuzwa mahindi kiasi cha Tani 64,477.95 zenye thamani ya Shillingi Billioni 90.6 za kitanzania na maharage Tani 99,434.45 zenye thamani ya Shillingi Bilioni 222.0 za Kitanzania.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo Dkt Charles Tizeba (Mb), jana tarehe 16 Octoba 2018 wakati akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani Kitaifa ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya JK Nyerere katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma.

Dkt Tizeba alisema kuwa mazao hayo yamekuwa yakiuzwa zaidi katika nchi za Kenya, Uganda, DRC, Rwanda, Burundi, Sudani Kusini na Uarabuni.

“Pamoja na kuuza mazao nje ya nchi, nchi yetu imekuwa ikitegemea kuagiza zao la ngano kutoka nje ya nchi kutokana na uzalishaji mdogo wa zao hilo hapa nchini. Serikali inatoa wito kwa wakulima hususani wa maeneo ambayo zao hili linalimwa na kukua vizuri waweze kuongeza maeneo ya uzalishaji na tija ili nchi iweze kupunguza utegemezi wa zao hili kutoka nchi za nje” Alikaririwa akisema

Alisema, Pamoja na uzalishaji mzuri wa chakula nchini, Lishe duni (utapiamlo) kwa jamii na kwa baadhi ya maeneo inaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuathiri maendeleo ya wananchi kiafya, kielimu na kiuchumi.

Aidha, ili kuyafikia malengo endelevu ya maendeleo (Sustainable Development Goals), alisema , Lishe ni moja ya muhimili muhimu wa kuwezesha kufikiwa kwa malengo yote 17 hivyo Serikali kwa kulitambua hilo, imeamua kujumuisha masuala ya lishe kuwa mojawapo ya maeneo ya kimkakati katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21.

Kadhalila, aliwataka wadau wote wa lishe nchini kushiriki na kuonyesha bayana mchango wao katika kukabiliana na utapiamlo.

Tarehe 16 ya mwezi Oktoba kila mwaka, Tanzania na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, huadhimisha Siku ya Chakula Duniani ambapo lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kukumbushana wajibu wa kila mmoja katika kupambana na njaa, kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu inayosema “Matendo yetu ni hatima yetu. Dunia bila njaa ifikapo 2030 inawezekana”. “Kaulimbiu hii inatutaka kufanya kazi kwa umahiri mkubwa ili tujitosheleze kwa chakula na kuwa na akiba ya kutosha kuendesha maisha yetu ya kila siku.” Alisisitiza Dkt Tizeba na kuongeza kuwa

“Pia kaulimbiu hii inatukumbusha kuacha kufanya mambo kwa mazoea na badala yake tutumie utalaamu katika kuongeza kuzalisha mazao  ya kilimo, mifugo na uvuvi.”

MWISHO.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter