Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana amewakaribisha wawekezaji kufanya biashara ya hewa ukaa na Serikali ya Tanzania.
Dkt. Chana ameyasema hayo Jijini Dodoma mara baada ya Taasisi ya Blue Carbon ya UAE na Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kusaini mkataba wa makubaliano (MoU).
Mkataba huo umelenga kuanzisha ushirikiano wenye lengo la kukuza usimamizi endelevu wa misitu, kukabiliana na ukame na kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi.
Amesema kwa miaka mingi, changamoto za usimamizi wa misitu ni ukosefu wa motisha kwa jamii na serikali ya kulinda msitu.
“Ni matumaini yetu kwamba yaliyomo katika mkataba wa makubaliano yatachangia juhudi za taifa za kukuza ulinzi wa misitu na usimamizi endelevu.”
Waziri Dkt. Chana ameishukuru serikali ya UAE kuingia mkataba huo ambao umefungua milango katika sekta hiyo muhimu na kusisitiza kuwa serikali imeipa kipaumbele katika upande wa hewa ukaa.
“Hewa ukaa ni eneo jipya na wakati umefika sasa wizara yangu na wizara ya mazingia kuangalia namna ya kuimarisha hili.
Rai yangu kwa wananchi ni kuwa tuna misitu ya vijiji, halmashauri, ya watu binafasi na ya hifadhi basi tuitunze na tuilinde maana tunapata mazao mapya ya misitu.”
Kwa upande wa Mwanamfalme na Mwenyekiti wa Taasisi ya Blue Carbon, Sheikh Ahmed Dalmook Al Maktoum amesema “ni heshima kubwa kusaini Mkataba huu na Serikali ya Tanzania.
Ushirikiano huu unawakilisha hatua muhimu katika kukuza mazoea ya usimamizi endelevu wa misitu na kupambana na mabadiliko ya tabianchi”
Naye Kamishna wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo alisema wakati umefika sasa kwa nchi zilizoendelea kuweka mchango wao kwa nchi zinazoendelea kupunguza gesi joto.
Amesema hatua ya kusaini makubaliano na Blue Carobon ni mwanzo wa utekelzaji wa shughuli hizo na kuwa kampuni hiyo itaanza mchakato wa kusajili kwa kuzingatia sheria zinazozingatia biashara ya hewa ukaa ya mwaka 2022.