Home BIASHARAUWEKEZAJI Hifadhi ya msitu asilia Matogoro ni utajiri na fursa iliyofichika ya kiutalii mikoa ya Kusini

Hifadhi ya msitu asilia Matogoro ni utajiri na fursa iliyofichika ya kiutalii mikoa ya Kusini

0 comment 92 views

Hifadhi ya Msitu Asili Matogoro yenye mandhari ya kuvutia ni kichocheo adhimu na muhimu cha kukuza utalii katika mikoa ya kusini hususan mkoa wa Ruvuma.

Hifadhi hiyo imebeba hazina kubwa ya kihistoria ikiwemo uwepo wa mapango makubwa yaliyotumika wakati wa vita ya majimaji.

Haya yamebainishwa na Naibu waziri wa maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula alipofanya ziara ya kujionea fursa za kiutalii zinazopatikana katika Hifadhi ya Msitu Asilia Matogoro iliyopo Wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma.

Aidha, hifadhi hii ya Msitu Asilia na milima yake imebeba jukumu kubwa la uhai na ustawi wa Watanzania kutokana na ukweli kuwa Hifadhi hii ni chanzo cha mito mitatu mikubwa na muhimu ambayo ni Ruvuma unaomwaga maji yake kwenye bahari ya Hindi, Luwegu ambao unachangia asilimia 19 ya maji kwenye mto Rufiji na kisha kuingia bahari ya Hindi, na Mto Luhira ambao ni chanzo cha mto Ruhuhu ambao unamwaga maji yake kwenye Ziwa Nyasa.

Kitandula ametoa wito kwa wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza katika eneo hilo lenye mandhari nzuri na ya kuvutia ambayo inafaa kwa utalii wa kupanda milima, utalii wa picha, utalii wa kuruka kwa puto na utalii wa ikolojia kukimbilia na kuikumbatia fursa hiyo.

Vilevile Kitandula ameutaka uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambao unasimamia eneo hilo kulitangaza kwa kuliunganisha na matamasha mbalimbali ya vijana yanayofanyika katika mkoa wa Ruvuma kwa kuwashawishi washiriki watembelee Hifadhi ya Msitu Asilia Matogoro.

“Nina uhakika mandhari niliyoiona hapa maharusi wengi wangetamani kufika kileleni na kufanyia sherehe zao za harusi mahali hapa,” amesema Kitandula.

Akihitimisha ziara yake, ameushukuru Uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano unaoutoa kwa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii hasa kwenye kukabiliana na changamoto ya wanyama wakali na waharibifu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter