Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema serikali inaendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo ili kuwajengea uwezo wa kufikia ngazi ya kuwa wachimbaji wa kati, hali ambayo itaongeza mapato pamoja na kuchochea ongezeko la ajira. Kairuki amesema hayo wakati akizungumza na wachimbaji wadogo katika kijiji cha Komoro wilayani Simanjiro ambapo ameongeza kuwa tayari serikali imeshakamilisha mchakato wa kurejesha ruzuku ambao ulisitishwa baada ya kugundulika kuwa sio wachimbaji wadogo pekee ndio waliokuwa wakinufaika nayo.
Kairuki ameeleza kuwa mchango wa sekta ya madini ni asilimia 4.7 pekee, kiwango ambacho amedai kuwa ni cha chini ikilinganishwa na wingi wa rasilimali pamoja na nguvu kazi. Waziri Kairuki pia amesema katika jitihada za kuendeleza sekta hiyo, serikali imebaini maeneo 44 maalum kwa wachimbaji wadogo na taratibu husika zitatumika kuyatoa.