Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema uzinduzi wa maabara ya kisasa ya kutambua vinasaba vya madini utasaidia kutokomeza biashara ya magendo ya madini. Majaliwa akizungumza katika uzinduzi huo amesema, maabara hiyo ambayo imegharimu zaidi ya Sh. 60 bilioni inatumia teknolojia ya kisasa na ni ya kwanza Afrika na ya pili duniani.
Ujenzi wa maabara hiyo umwezeshwa kwa ushirikiano wa kampuni ya utafiti ya kijiolojia ya Ujerumani (BGR) na Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).Waziri Mkuu ameeleza kuwa mbali na kufanikisha mradi huo, serikali imefanya marekebisho kwenye baadhi ya Sheria za madini ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa wazi zaidi na taifa linanufaika na rasilimali zake.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa wizara ya madini Prof. Simon Msanjila amesema baada ya vipimo, madini yote yatakayoonyesha shaka hayatokubaliwa na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika. Naye Makamu wa Rais wa BGR Volker Steinbach amesema maabara hiyo itafanikisha uhakiki bora zaidi wa madini.