Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Injinia James Kilaba amesema Mfumo wa Usimamizi wa Mawasiliano ya Simu (TTMS) utarahishisha usimamiaji wa masuala mbalimbali hususani katika ukusanyaji wa mapato hivyo kuiwezesha nchi kupiga hatua zaidi kiuchumi.
Mkurugenzi huyo amesema hayo wakati akitoa taarifa kuhusu mfumo huo, katika makabidhiano yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa, TCRA inafanya kazi kwa karibu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambapo mfumo huo utawasaidia kukusanya taarifa muhimu za wateja wao kwa kutumia simu za mikononi.
“Mfumo huu una faida sana katika nchi yetu lakini hasa katika ukusanyaji wa mapato kwa sababu utawezesha kutambua vyanzo vya mapato ya watoa wa huduma za fedha kwa njia ya simu na itawasaidia TRA kufanya kazi zao kwa urahisi”. Amesema Injinia Kilaba.
Aidha, Mkurugenzi huyo ametaja faida nyingine za mfumo huo kuwa ni: utawezesha kupatikana takwimu za mawasiliano yanayofanyika ndani na nje ya nchi, kupata na kugundua mawasiliano ya simu za ulaghai pamoja na kutambua ada za huduma za fedha mtandaoni.
97