Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Mikataba ya Uwekezaji wa Bandari iliyosainiwa imezingatia maoni yaliyotolewa kupitia makundi mbalimbali ya kijamii, pamoja na sheria na taratibu zote za nchi.
Rais Samia ameyasema hayo Oktoba 22, 2023 wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba mitatu ya uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na serikali kampuni ya DP World Dubai iliyofanyika Ikulu, Chamwino Dodoma.
Ameeleza kuwa, serikali ilisikiliza maoni mbalimbali yaliyotolewa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, vyama vya siasa, asasi za kiraia, wanaharakati, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, viongozi wa dini na baadhi ya viongozi wastaafu.
“Mikataba iliyosainiwa imetokana na makubaliano ya awali kati ya serikali na Mamlaka ya Dubai ambao wameridhia mahitaji na matakwa ya nchi kama yalivyoanishwa kwa kuzingatia maslahi ya taifa,” amesema Rais Samia.
Amebainisha kuwa mikataba iliyosainiwa ni Mkataba wa Nchi Mwenyeji (Host Government Agreement), Mkataba wa Upangishaji Ardhi (Leas Agreement) na Mkataba wa Uendeshaji wa Bandari (Concession Agreement).
“Uimarishwaji utakaofanywa kupitia uwekezaji huu utakuza biashara za ndani na nje pamoja na kuwezesha shughuli za kiuchumi za nchi jirani hivyo kuongeza mapato ya serikali na kukuza uchumi wa taifa,” ameeleza Rais.
Amesema mikataba hiyo mitatu imesainiwa kwa kuzingatia Kifungu cha 2 cha Sheria ya Ubia Namba 6 ya mwaka 2023 (the Public Private Partnership Act CAP 103) na Kifungu cha 2 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Namba 5 ya mwaka 2023 (the Public Procurement Act No 5 of 2023).