Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk. Charles Mhina amesema serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (LIC) wameanza kutekeleza miradi 47 ya uwekezaji iliyopo mikoa ya Dodoma na Kigoma.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa miradi hiyo inatekelezwa ili kuboresha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, miundombinu ya masoko, minada, machinjio na utafiti wa vyanzo vya maji na viwanda vidogo. Ameeleza kuwa wanategemea kuwanufaisha watu takribani 18,896 kati yao ni wanawake 6,586 na wanaume 12,310.
Kupitia mradi huo Dk. Mhina amesema wakulima na wafugaji wapatao 1,500 wameshanufaika kwa kujifunza ujasiriamali, kuandikia miradi kwa maandishi na kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili waweze kujipatia mikopo.
“Kwa sasa mradi unaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi, upimaji na utoaji hati katika miradi mikubwa ya uzalishaji kupitia kilimo cha umwagiliaji na makazi katika Halmashauri za Wilaya ya Kasulu na Uvinza mkoani Kigoma na zile za Bahi na Kondoa mkoani Dodoma”. Amesema Dk.Mhina na kuongeza:
“Kukamilika kwa mradi huu unaogharimu zaidi Shilingi milioni 596.33 na tunatarajia wakulima na wafanyabiashara zaidi ya 9,266 watanufaika”.