Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel (Sekta ya mifugo) amezungumza na Kaimu Balozi wa Misri nchini, Nevine El-Saeed na kupokea andiko la awali la nia ya Misri kutaka kuwekeza katika sekta ya mifugo hapa nchini. Prof. Gabriel ameeleza kuwa Tanzania imebarikiwa na mifugo mingi na ikitumika vizuri, hususani kupitia sekta ya uwekezaji, fursa nyingi zaidi zikiwemo za ajira. Katibu huyo amesema nia yake ni kuhakikisha anasimamia kwa uweledi nia ya serikali ya Misri na kufanikisha uwekezaji huo ambao amesisitiza wizara yake itahakikisha inaandaa mazingira rafiki yatakayopelekea uwekezaji huo kuwa endelevu na kuleta tija kwa pande zote mbili.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amesema nia yake ni kuhakikisha anasimamia nia ya serikali ya Misri kufanikisha uwekezaji huo ambao anasema wizara yake itahakikisha inaweka mazingira yatakayofanya uwekezaji huo uwe endelevu na kuleta tija kwa nchi zote mbili. Kwa upande wake, Kaimu Balozi El-Saeed ambaye aliambatana na Mkuu wa Idara ya Uchumi katika ubalozi huo, Mohamed Ibrahim amesema serikali ya Misri imedhamiria kuwekeza ili kuzalisha fursa mbalimbali kupitia uwekezaji huo.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni wakuu wa idara zilizo chini ya ofisi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wawakilishi kutoka Dawati la Sekta Binafsi, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Kituo cha Kuendeleza kilimo Nyanda za juu Kusini (SAGCOT) na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki.