Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko ameagiza wawekezaji wa mgodi wa Magambazi uliopo wilayani Handeni mkoani Tanga kutoa taarifa za mikataba yao na fedha walizolipana ndani ya wiki moja kutokana na hali ya sintofahamu iliopo baada ya wawekezaji hao kuuziana mgodi huo. Waziri Biteko amesema badala ya wawekezaji hao kuisababishia wilaya na serikali kwa ujumla hasara, ni bora wafutiwe leseni.
Waziri Biteko ameeleza kuwa anataka taratibu zote walizoingia wawekezaji hao ambao ni kampuni ya Canaco pamoja na Tanzania Goldfields pamoja na fedha walizolipana, namna wanavyofanya kazi pamoja na uharibifu unaotokana na kazi zao kufahamika ndani ya siku saba alizowapatia.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe amesema kushindwa kufanya kazi kwa wawekezaji wa mgodi huo kunaigharimu serikali zaidi ya Sh. 1.3 bilioni huku akimuunga mkono Naibu Waziri na kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya wawekezaji hao.