Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel ametoa wito kwa benki ya NMB kushirikiana na wizara hiyo ili kukuza sekta ya maziwa hapa nchini kwani kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Chakula Duniani (WFP), bado kuna mwitikio mdogo wa wananchi kunywa maziwa.
Prof. Gabriel ameeleza hayo katika kikao na maafisa kutoka Idara ya kilimo ya NMB, waliofika ofisini kwake kueleza mikakati ya benki hiyo ambayo imekuwa ikifanya tafiti na wadau wa sekta ya maziwa na kuonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika sekta hiyo.
“Kwa takwimu ambazo zimetolewa na Shirika la Chakula Duniani ni kwamba kwa wastani angalau mtu anatakiwa walau atumie lita mia mbili kwa mwaka za maziwa lakini kwa bahati mbaya kwa watanzania wastani ni lita arobaini na saba tu, bado tuna kazi kubwa sana”. Amesema Katibu huyo.
Mbali na hayo, Prof. Gabriel pia amesisitiza umuhimu wa tafiti kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na NMB ili tafiti hizo zifanyiwe kazi na kuleta tija kwa wafugaji.
Naye Meneja Mwandamizi wa NMB kutoka Idara ya kilimo Carol Nyagaro amesema kasi ya serikali inayoongozwa na Rais Magufuli pamoja na utendaji wake imepelekea benki hiyo kubadili mtazamo wa kutafuta wateja.
“Kutokana na kasi ya Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli na uongozi mzima wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwetu inajenga mazingira mazuri ya kufanya biashara, pia kuchangia maendeleo ya jamii na kuweza kutengeneza wateja wa siku zijazo”. Amesema Ngayaro