Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete ameusifia mradi wa kufua umeme kwa njia ya maji wa Mwalimu Nyerere uliochwa na Rais wa awamu ya tano Hayati John Pombe Magufuli.
Rais Kikwete, Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi pamoja na viongozi wengine wametembelea mradi huo wa megawati 2115 unaotarajiwa kukamilika June, 2022.
“Kwanza mimi nashangaa tuu, kwa sababu nimehusika na kujenga power station mbili kipindi nilichokuwa waziri lakini hazikuwa kubwa kama hizi, kwa hiyo ukiangalia ukubwa wa hii power station na kazi kubwa iliyofanyika ni kazi kwa kweli ya sifa kubwa, ni kazi inayostahili pongezi,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ametoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Tano iliyokuwa chini ya Hayati Rais Magufuli kwa kuonesha uthubutu kwa kuanzisha ujenzi wa mradi huo ambapo ameshauri Wizara ya Nishati kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa fursa zitakazoambatana na kukamilika kwake.
Amesema “nina uhakika Rais Samia Suhulu Hassan, atahakikisha mradi huu unakwenda sambamba na matarajio ya mtangulizi wake na kukamilika kwa wakati.”
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa mradi huo, kutakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa nzima kwa ujumla.