Home BIASHARAUWEKEZAJI Serikali yataka ubunifu wa Watanzania ulindwe

Serikali yataka ubunifu wa Watanzania ulindwe

0 comment 116 views

Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imetaka ubunifu wa Watanzania ulindwe na kuendelezwa.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo Exaud Silaoneka Kigahe amesema vijana wengi Watanzania wana ubunifu lakini bunifu hizo huchukuliwa na watu wengine kutokana na kutolindwa kisheria.

Ameeleza kupitia taasisi za Wizara ambazo ni Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (Tanzania Industrial Research Development Organization – TIRDO) ambao wanasaidia wabunifu, pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Business Registrations and Licensing Agency – BRELA) ambao wanasajili makampuni mbalimbali lakini pia kulinda bunifu mbalimbali itahakikisha bunifu za Watanzania zinalindwa.

“Tunafikiri sasa tuanze kulinda bunifu miliki za vijana wetu sababu wengi wa vijana wana ubunifu lakini sera zetu kidogo bado hazijawaona ili kufaidika na ubunifu huo,” amebainisha Naibu Waziri katika Mkutano wa Nishati (Tanzania Energy Congress) jijini Dar es Salaam.

Aidha, amesema Wizara inahamasisha kuona Watanzania wanaingia au kuchangia uzalishaji na uongezaji wa thamani katika bidhaa mbalimbali ikiwemo kwenye mazao ya kilimo.

“Kupitia Taasisi zetu ambazo ni za kiteknolojia na kushirikiana na Taasisi za ubunifu, tunataka kuona namna ya kuwawezesha wawekezaji na wajasiriamali wa Tanzania ambao wana fursa kubwa zaidi ya kufaidi rasilimali tulizonazo kwenye sehemu ya nishati.

Kwa sasa tunahamasisha kwenye nishati jadilifu (renewable energy) ambapo tunalenga zaidi kwenye solar na umeme wa upepo na kurejelesha taka (recycle) kuweza kuzalisha nishati,” amesema.

Ameeleza kuwa ili Watanzania waweze kufanikiwa katika hilo ni lazma Serikali iwawezeshe kimtaji na sera madhubuti.

“Sisi kama Wizara tunapitia sera yetu ya uwekezaji lakini pia sera zingine zinazohusiana na ujasiriamali.

Moja ya sera tunayotaka tuiunde sasa ni sera ya ubora (Quality Policy).

Hii inalenga kuona tutawezaje kuzalisha bidhaa ambazo zitakuwa na ubora kushindana na bidhaa nyingine kwa maana hata katika uzalishaji wa nishati tuweze kuwa shindani badala ya kuwasaidia tuu wawekezaji kutoka nje tuweza pia kuwasaidia wa ndani waweze kufaidika na rasilimali tulizonazo kama nchi.”

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter