Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila, ametoa wito kwa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kutumia vizuri mtambo wa kuchoronga miamba ili kuleta tija kwa taifa. Prof. Msanjila amesema hayo katika hafla ya kukabidhi rasmi mtambo huo kwa Stamico na kueleza kuwa kununua mtambo huo ambao umegharimu Dola za Marekani 1.3 Milioni ni uwekezaji mkubwa hivyo shirika hilo linapaswa kuutumia kuleta manufaa.
Aidha Katibu Mkuu huyo ameitaka Stamico kujitangaza ipasavyo ili wananchi hasa wadau wa sekta ya madini wanaojishughulisha na uchimbaji na utafutaji, kufahamu uwepo wa mtambo huo ili utumike hata kwa kampuni binafsi kujiongezea kipato na kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa ujumla.
“Kwa zabuni nilizozisikia mpaka sasa mtambo huu utazalisha pesa za kutosha”. Amesema Prof. Msanjila.
Pamoja na hayo, Katibu huyo pia ameagiza shirika hilo kuhakikisha mtambo huo unawezesha ununuzi wa mtambo mwingine mpya kila mwaka, ili ndani ya muda wa miaka mitano, shirika liweze kumiliki mitambo mitano, hivyo kurahisisha shughuli za uchimbaji na utafutaji wa madini.