Home BIASHARAUWEKEZAJI Serikali kuweka mazingira safi kuvutia wawekezaji

Serikali kuweka mazingira safi kuvutia wawekezaji

0 comment 92 views

Serikali ya Tanzania imekuwa ikichukua hatua za makusudi katika kuandaa mazingira bora ya kuwavutia wawekezaji nchini ili kuweza kutimiza azma yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya viwanda kupitia sera ya “Tanzania Ya Viwanda”

Siku chache zilizopita, serikali ya Tanzania imeihakikishia Serikali ya Norway kuwa inaendelea kuelekeza nguvu zake kwenye kuweka mikakati ya kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga, ametoa ahadi hiyo alipokutana na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD), Jon Lamoy, mwanzoni mwa ziara yake ya kikazi ya siku tatu mjini Oslo, Norway.

Katika mazungumzo yao, Lamoy amemueleza Waziri Mahiga kuwa, shirika hilo limekuwa na uhusiano wa karibu na wa kindugu kwa zaidi ya miongo mitano na Tanzania.

Ameongeza kuwa yeye na washirika wengi wa Tanzania nchini humo wanasifu utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli hasa kwenye mapambano dhidi ya rushwa.

“Rushwa inarudisha nyuma maendeleo kwa kuikosesha nchi mapato, hivyo jitihada za Tanzania za kupambana na rushwa, hususan kwenye ukusanyaji kodi, zitawawezesha wananchi wa Tanzania kunufaika na huduma za kijamii, hatimaye kupata maendeleo kwa haraka,” amesema.

Mbali na hayo, Mkurugenzi huyo alitoa angalizo kuwa nia nzuri ya serikali ya Tanzania ya kuweka mifumo thabiti ya uwekezaji wenye faida ukiwemo ule wa sekta ya madini, ni muhimu ikakamilika mapema ili kutoa fursa kwa wawekezaji wapya kuwekeza kwenye sekta hiyo kwa wakati.

Mahiga alielezea kuwa suala hilo tayari linafanyiwa kazi ambapo pamoja na serikali kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, uwekezaji huo ni lazima uwe na faida kwa watanzania na kwa maendeleo ya nchi.

Kwenye mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk. Wilbrod Slaa kwa pamoja walielezea kuwa marekebisho hayo, yatakapokamilika, yatabadili mazingira ya uwekezaji Tanzania.

Awali, kabla ya mkutano huo Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa kampuni ya Statoil yenye makao yake makuu Mjini Oslo, ambayo kwa sasa nchini humo inajulikana kama Equinor.

Makamu wa Rais Mtendaji wa kampuni ya Statoil Lars Christian Bacher alielezea shughuli za kampuni hiyo Tanzania ikiwemo kujenga uwezo wa ndani ya nchi kwa watanzania kuijua na kuendesha sekta hiyo muhimu kwa ukuaji wa uchumi. Alisema kwa sasa kampuni hiyo inatoa ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili kwa Watanzania 10 kila mwaka kwenye eneo la mafuta na gesi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter