Ubalozi wa Uingereza na Serikali ya Tanzania wanatarajia kufanya kongamano la pili la kibiashara kutambua fursa za kibiashara na uwekezaji utakaosaidia kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi.
Akizungumza katika uzinduzi wa kongamano hilo Novemba 29 jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Ally Gugu amesema kongamano hilo litawaleta pamoja wafanyabiashara zaidi ya 100 kutoka Tanzania na Uingereza.
Amesema wafanyabiashara hao watatambua fursa za biashara na uwekezaji katika kubadilishana maarifa juu ya kufanya biashara nchini ambapo ni fursa kwa Tanzania kuongeza mauzo ya nje ya nchi kwenda Uingereza.
“Kwa kuzingatia ahadi kutoka katika kongamano la mwaka jana, kwa mwaka huu tutajumuisha vikao kadhaa vya kupeana taarifa na mijadala.
Pia kutakuwa na jopo inayohusisha wataalam wa biashara na uwekezaji, kusaidia kuboresha mazungumzo kati ya serikali na sekta binafsi ili kuongeza imani ya uwekezaji na biashara,” amesema.
Gugu aliwataja watakaoongoza kongamano hilo kuwa ni Mjumbe wa Waziri Mkuu wa Uingereza wa biashara nchini Tanzania, Lord Walney na Waziri wa nchi, Ofisi ya rais, kazi, uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mudrik Ramadhani Soranga.