Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amesema kuzinduliwa kwa Tume ya Madini ni ishara kuwa sekta ya madini imedhamiria kubadili historia. Tume hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuleta mapinduzi na kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na rasilimali zinazowazunguka. Kairuki ameeleza kuwa mbali na kupewa mamlaka makubwa, tume hiyo pia inabeba jukumu la kuhakikisha inatekeleza kikamilifu usimamizi, udhibiti, ukaguzi, ufuatiliaji, ukusanyaji wa taarifa pamoja na kuweka kumbukumbu kwa kusimamia sekta hiyo kwa uadilifu ili kusaidia taifa kunufaika na uwepo wa rasilimali ya madini.
Ameongeza kuwa watanzania wana matarajio makubwa na tume hiyo na wanaamini sekta ya madini ipo katika mikono salama. Tume ya Madini imeundwa kama sehemu ya juhudi za Serikali ya awamu ya tano kuhakikisha kuwa rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote. Tume hiyo imebeba jukumu la kusimamia sekta ya madini huku Wizara ya madini ikiendelea kusimamia masuala ya kisera.