Serikali ya Tanzania imetoa wito kwa wawekezaji kutoka Ufaransa kuwekeza katika viwanda vya bidhaa za kilimo na kuangazia soko kwa ajili ya bidhaa mbalimbali za vyakula nchini kwao ili kuimarisha mahusiano ya kibiashara baina ya nchi hizo mbili.
Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Dkt.Charles Mwijage amesema wakati ujumbe wa sekta binafsi kutoka Ufaransa (MEDEF) ukihitimisha ziara ya siku tatu ya kuangalia fursa za uwekezaji kuwa, ni fursa ya kipekee kwa nchi hiyo ambayo ina mafanikio makubwa kibiashara kufika hapa kwetu na kuangalia fursa za uwekezaji.
MEDEF wanashirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) na kuangazia maeneo muhimu ya kuwekeza ili kuleta maendeleo. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPSF Dk. Reginald Mengi amesema kuna fursa mbalimbali za uwekezaji hapa nchini na wakati umefika kwa wafanyabiashara wazawa kufaidika na fursa hizo.