Home BIASHARAUWEKEZAJI Wananchi watakiwa kuwa na mahusiano mazuri na wawekezaji

Wananchi watakiwa kuwa na mahusiano mazuri na wawekezaji

0 comment 65 views

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amezitaka jamii zinazonguka maeneo ya migodi kutangaza mazuri yanayofanywa na wawekezaji katika sekta ya Madini ili kuwatia moyo wa kufanya shughuli za madini.

Dkt. Biteko ameyabainisha hayo, Julai 22, 2022 akiwa katika ziara yake kijiji cha Kagerankanda wilaya ya Kasulu alipotembelea mgodi wa Kampuni ya Life Business unaochimba madini ya Chokaa mkoani Kigoma.

Amesema, migogoro baina ya wawekezaji katika Sekta ya Madini na wananchi katika maeneo mengi ya migodi imewafanya wawekezaji kupata hofu ya kuwekeza katika uchimbaji wa madini katika baadhi ya maeneo na hivyo kupunguza uzalishaji.

Amewataka wananchi kuhakikisha wanajenga mahusiano mazuri na wawekezaji ili kutatua changamoto zinazojitokeza kati yao ili wawekezaji waweze kutekeleza huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo yanayozunguka migodi.

Aidha, Dkt. Biteko ameahidi kuwa changamoto zilizopo ikiwemo ukosefu wa barabara na ujenzi wa madarasa zitafanyiwa kazi haraka baada ya kutoa maelekezo kwa mwekezaji huyo.

Kwa upande wake, mmiliki wa mgodi huo ndugu Lister Balegele ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) amesema, Kampuni hiyo imekuwa ikilipa mapato ya Serikali na michango mbalimbali kutokana na mauzo ya madini ya chokaa.

Kuhusu huduma za kijamii Balegele amesema, mgodi unajenga madarasa mawili mpaka sasa katika shule ya sekondari hapo kijijini, wametoa madawati 50 kwa ajili ya shule pamoja na kugawa kompyuta mpya kwa shule ya sekondari na msingi.

Baada ya ziara ya Dkt. Biteko katika mgodi huo, mwekezaji wa mgodi huo ameahidi kukamilisha barabara na ujenzi wa madarasa hivi karibuni.

Naye, Mjiolojia Mwandamizi kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) John Kalimenze amesema, Serikali kupitia taasisi hiyo itaendelea kufanya tafiti za madini ili iweze kugundua maeneo zaidi kwa ajili ya uchimbaji na kuongeza tija kwa wachimbaji na kuongeza mapato ya Serikali.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter