Wawekezaji wametajwa kuwa moja ya wadau muhimu kwa ustawi bora wa uchumi wa Tanzania na kufungua fursa za ajira kwa Watanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu amebainisha hayo Agosti 11 jijini Dar es Salaam katika Jukwaa la Wafanyabiashara wa Afrika Kusini waliopo hapa nchini.
Kupitia jukwaa hilo, wafanyabiashara wameonesha nia ya kuwekeza katika Sekta ya Nyumba nchini.
Mchechu amesema lengo la ushiriki wake katika mkutano huo ni kuwapitisha wafanyabiashara hao katika malengo na mikakati ya shirika ambayo inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
“Tunaamini wawekezaji ni muhimu sana, na sisi tunatembea katika mapito ya Royal Tour kwa kutangaza fursa na kuwaleta wawekezaji na NHC tuna mikakati mipya sasa hivi, ambayo tumeipanga.
“Kwa kushirikiana na sekta binafsi tunaanza miradi mipya Dar es Salaam ndani ya mwezi ujao wa tisa na tutaendelea kumalizia miradi ambayo ilikwama kidogo,” ameeleza Mchechu.
Mchechu amebainisha kuwa NHC imejiwekea malengo ya kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya nyumba nchini.
“Tunaamini kwamba nyumba ni muhimu sana kama ilivyo chakula, kwa Dar es Salaam kuna miradi ambayo tutaifanya sisi wenyewe na mingine kupitia sekta binafsi kwa maana ya Public- Private Partnerships (PPPs).
Amesema, hatua hiyo ina lengo la kuharakisha uendelezaji wa maeneo yaliyo wazi katikati ya miji kwa kujenga nyumba za vitega uchumi na hivyo kuliongezea shirika na nchi mapato makubwa.
“Sisi tunajenga nyumba za kuuza, kupangisha na niseme tunajenga kwa watu wote hata tunapofanya maendelezo ya ubia kipaumbele kinaanza kwa yule ambaye anakaa kwenye ile sehemu, lakini siyo kwamba yeye ndiye mwenye haki pekee, kama anakuwa hajisikii basi huyo unamsaidia Mtanzania mwingine kwa sababu uhaba wa nyumba ni mkubwa kuliko unazoziona (zilizopo),” amesema Mchechu.
Mkurugenzi huyo amesema, vipaumbele hivyo ni pamoja na kutekeleza mpango wa ujenzi wa nyumba 5000 za gharama ya kati ujulikanao Samia Housing Scheme (SHS).
Mchechu amesema 50% ya nyumba hizo zitajengwa jijini Dar es Salaam, huku 20% zitajengwa Dodoma na 30% katika mikoa mingine nchini.
Mkurugenzi huyo aliupongeza Ubalozi wa Afrika Kusini hapa Tanzania kwa kuendelea kuwashirikisha fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania wawekezaji kutoka nchini humo.
Kaimu Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Stella Vuyelwa Dhlomo-Imieka amesema kuwa licha ya Tanzania na Afrika Kusini kuwa na uhusiano mwema na ushirikiano wa muda mrefu, wataendelea kuitumia diplomasia ya uchumi ili kuhakikisha wanawakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo kuja kuwekeza Tanzania.
Amesema kuwa ushirikiano wa kiuchumi ni chachu kubwa ya kuyafikia malengo ya kuimarisha na kuharakisha maendeleo, na sekta ya nyumba ni miongoni mwa maeneo muhimu.