Home BIASHARAUWEKEZAJI Wizara ya Madini yaanza kutangaza fursa za uwekezaji kwenye madini nchini China

Wizara ya Madini yaanza kutangaza fursa za uwekezaji kwenye madini nchini China

0 comment 96 views

Na Grace Semfuko-MAELEZO.
Wizara ya Madini imeanza mkakati wa kutangaza fursa za uwekezaji wa sekta hiyo nchini China ili kuvutia wawekezaji wa China kuja kuwekeza nchini kwa teknolojia ya hali ya juu ambayo itaimarisha uzalishaji katika sekta hiyo na hivyo kuongeza pato la taifa.

Miongoni mwa maeneo yatakayopata fursa ya kutangazwa ni pamoja na mradi wa kuzalisha umeme wa makaa ya mawe ya Kiwira, mradi wa dhahabu wa madini wa Buhemba unaoshikiliwa na shirika la Madini la Taifa STAMICO, pamoja na kuelezea huduma mbalimbali za Kisheria, Sera na Kanuni mbalimbali za uwekezaji wa madini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam kuhusiana na ziara yake ya nchini China kuhudhuria kongamano maalum baina ya China na Tanzania la kuvutia wawekezaji wa Sekta ya Madini litakalofanyika Desemba 10-14 mwaka huu, Waziri wa Madini, Angella Kairuki amesema Tanzania itaitumia fursa hiyo kuvutia wawekezaji.

“Tunaenda kuitangaza miradi ya aina mbili, ikiwepo miradi ya Serikali ya kuzalisha umeme unaotokana na makaa ya mawe, Kiwira, uliopo Rungwe, Mkoani Mbeya, mradi wa Madini ya dhahabu wa Buhemba, uliopo Mkoani Mara, kadhalika miradi mbalimbali inayoshikiliwa na STAMICO, pia tutaelezea huduma mbalimbali za madini na kutoa ufafanuzi wa Sheria , Sera na kanuni za uwekezaji katika sekta ya madini maana kuna watu wamekuwa wakileta upotoshaji mkubwa,” Alifafanua Waziri.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania – TIC, Geoffrey Mwambe, ambaye alishiriki katika mkutano huo na waandishi wa habari, alisema kazi ya kuvutia wawekezaji inafanywa ili kuimarisha uchumi wa Taifa, kutokana na kodi itakayopatikana, pia kuongeza nafasi za ajira zitakazotokana na uwekezaji huo, na aliwataka watendaji wa Serikali kutotenda vinginevyo, badala yake wafuate Sheria pale inapobainika wawekezaji wamefanya makosa.

“Kazi hii ya kuvutia uwekezaji ni kubwa mno, lengo letu ni kuhakikisha sekta hii inaliingizia Taifa letu fedha zitakazotokana na tozo mbalimbali, watendaji, … wenzangu ni muhimu tukazingatia Sheria pale inapobainika kuna kasoro zinazofanywa na wawekezaji, tusijichukulie hatua mkononi, tunatumia ushawishi mkubwa sana kuwaleta na hivyo tutumie njia sahihi za kurekebisha kasoro zao,” alisema Mwambe.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wachimbaji Madini Tanzania, Bw. John Bina, alisema hatua ya Serikali ya kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini itasaidia kuimarisha sekta hiyo kiuchumi kwani sasa madini yanayochimbwa bado hayajaweza kutosheleza mahitaji.

“Tunachimba madini kwenye maeneo machache sana, tukiongeza wawekezaji angalau tutakuwa na eneo kubwa ambalo litaimarisha uchumi, kwa nchi ya China tunategemea sana teknolojia zao ambazo zinauzwa kwa bei rahisi hivyo wakija nchini tutapata ujuzi zaidi pamoja na matumizi ya mashine zao za kisasa ” alisema Bina.

Ziara hiyo imeandaliwa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Msafara wa Tanzania ambao washiriki wanatoka Taasisi za Serikali na wadau wa sekta binafsi waliowekeza katika sekta ya madini jumla yao ni washiriki 80, wakitoka makampuni 44 ya Tanzania na vyama 2 vya Wafanyabiashara, wawekezaji katika sekta ya madini nchini China wamethibitisha kushiriki kongamano na kwa upande wa Serikali yao jumla ya taasisi 6 zinazotoa huduma mbalimbali kwa wawekezaji wa sekta ya madini imeelezwa zitashiriki kongamano.

Aidha katika kongamano hilo ya kampuni 35 zinazojihusisha uwekezaji na biashara mbalimbali ya sekta ya madini kwa upande wa China zitashiriki.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter