Home BIASHARA Vidokezo 5: ikiwa unataka kupanua biashara yako

Vidokezo 5: ikiwa unataka kupanua biashara yako

0 comment 114 views

Ni dhahiri kuwa kila mfanyabiashara anaeanzisha biashara au ambaye ameshaanzisha biashara ana malengo ya kuipanua biashara hiyo ili kuweza kupata mafanikio zaidi. Ieleweke kuwa kuanzisha biashara ni mchakato mwingine, na kupanua biashara ni mchakato tofauti unaokuja na majukumu zaidi, changamoto mpya, faida na mengineyo ndio maana ni muhimu kwa kila mfanyabiashara kutafakari kwa kina kabla ya kufanya maamuzi ya kupanua biashara yake ili kuiweka biashara hiyo katika upande sahihi.

Mambo ya kuzingatia;

Muda na Wateja

Muda ni jambo muhimu sana katika biashara. Ikiwa mfanyabiashara ataamua kupanua biashara yake katika muda usio sahihi basi atakuwa anaiweka biashara yake katika hatari au hali mbaya. Hiyo mfanyabiashara atajuaje kuwa ni muda sahihi? Jibu hapa ni ‘wateja’. Hivyo basi mfanyabiashara anatakiwa kuangalia msingi uliopo katika upande wa wateja kwenye biashara yake. Kwamfano, je katika biashara hiyo kuna wateja wengi wa kuaminika? Wateja wengi wanaridhishwa na ubora wa bidhaa au huduma hiyo? Pia uhitaji wa bidhaa au huduma hiyo ni mkubwa kiasi gani? Je kuna wateja ambao wanatoka mbali au wanaagiza bidhaa kutoka maeneo ya mbali? Kwa kujua majibu ya maswali haya na mengine kutokana na biashara yako itakuwa rahisi kuamua kama muda umefika wa kupanua biashara yako ili kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi na kupata mafanikio.

Wafanyakazi

Ikiwa umewaajiri wafanyakazi hakikisha wafanyakazi wako ni hodari, na wachapa kazi ipasavyo kabla ya kupanua biashara yako. Kwasababu ni muhimu kwa wafanyakazi pia kuwa tayari kwa mabadiliko yatakayotokea. Upanuzi wa biashara huja na majukumu zaidi, changamoto zaidi, na hata muda wa kazi unaweza kuongezeka hivyo hakikisha kuwa wafanyakazi wako katika upande wako na wana utayari wa upanuzi huo.

Mtiririko wa fedha

Upanuzi wa biashara huja na gharama zake, hivyo pitia fedha zilizopo katika biashara yako ili kuweza kujua kama utaweza kumudu gharama za upanuzi wa biashara yako. Ndio maana siku zote huwa inashauriwa kurekodi na kupitia mapato na matumizi ili kuweza kujua kama mtiririko wa fedha unakwenda sawa au la.

Bidhaa au huduma zinazohusiana

Ikiwa unauza bidhaa ambazo zinaingiliana na bidhaa nyingine na wateja wana uhitaji nazo basi huo ni muda muafaka wa kupanua biashara yako ili kuweza kukidhi mahitaji ya wateja wako. Kwani wateja wengi hufurahia zaidi sehemu ambazo wanaweza kupata bidhaa mbalimbali kwa wakati mmoja hii huwaepushia upotevu wa muda na gharama za kufuata kila bidhaa mahali pake.

Mfumo wa uendeshaji

Ikiwa biashara yako ina mfumo maalum wa uendeshaji basi ni rahisi kupanua biashara hiyo ikawa kubwa zaidi. Ndio maana inashauriwa kugawanya majukumu katika biashara yako kutokana na bajeti yako ili kuweza kupata matokeo makubwa zaidi kwani kila mtu huleta ujuzi na utaalamu wake na kwa pamoja hutengeneza matokeo makubwa zaidi ambayo yakipelekwa sokoni ni rahisi kuwavutia wateja wengi zaidi. Hivyo kama bado unafanya kila kitu mwenyewe na huna mfumo maalum wa uendeshaji wa michakato mbalimbali katika biashara yako basi muda unaweza kuwa sio sahihi kufanya upanuzi wa biashara yako.

Aidha, kutokana na biashara yako unatakiwa kuwa tayari kuwekeza muda na juhudi ili kuweza kuifikisha biashara yako mahali unapotaka ifike. Pia ni muhimu kufanya mambo kulingana na uwezo wako ili kujiepusha mambo yoyote yanayoweza kutokea mbeleni kwamfano unaweza kuchukua mkopo ambao unaweza kuulipa hata ikitokea upanuzi wa biashara yako haujaenda vizuri ili  athari itakayotoea isiathiri biashara nzima.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter