Hata katika biashara ndogo, ni muhimu kuwa na uongozi ili kurahisisha usimamizi wa majukumu yaliyopo. Kiongozi mzuri ni yule ambaye anaweza kuwaongoza watu katika muelekeo unaotakiwa na kufanya maamuzi yatakayosaidia biashara kufikia malengo yake.
Mtu yoyote anaweza kuwa kiongozi hata kama anajiongoza yeye mwenyewe. Siku zote kiongozi bora ni yule anayeongoza kwa vitendo na sio maneno. Hilo linawezekana kwa kuwa na mipango madhubuti katika kila jambo linalofanyika na linalotakiwa kufanyika mbeleni. Kipindi kigumu ndio muda sahihi wa kujipima kama wewe ni kiongozi bora au la kwa sababu kiongozi haogopi changamoto na hutoa suluhisho kwa changamoto zozote zinazoweza kuathiri biashara.
Siku zote kiongozi bora huwa na maono. Hii huleta muelekeo katika biashara. Kama kiongozi au viongozi katika hawana maono biashara haiwezi kufika mbali na kutakuwa hakuna maana ya kutengeneza au kuunda mipango. Kama kiongozi ni muhimu kuwashirikisha wafanyakazi wengine ili kuhakikisha kila mtu anatekeleza upande wake na kuhakikisha malengo ya biashara yanatimia.
Kama kiongozi unatakiwa kutambua nafasi yako na kuhakikisha wakati wa utekelezaji wa majukumu unakuwa mstari wa mbele kuhakikisha mipango inafanyika, unafanya maamuzi kutokana na hali ilivyo bila kujali hisia na kuhakikisha vitendo vinafanyika zaidi kuliko maneno.
Kiongozi mwenye nguvu siku zote huhamasisha kwa mifano. Biashara ni ya kwako na hakuna mtu ambaye ataijali kama wewe. Hivyo ili kuhakikisha majukumu yanakwenda kama inavyotakiwa ni muhimu kwa watu wengine kuona kuwa una uwezo wa kuwajibika na unajua kwanini ulianzisha biashara hiyo na wapi unataka ifike. Kwa kufanya kazi kwa bidii, hata wale unaowaongoza wataiga mfano wako.
Unaweza kujifunza kuwa kiongozi mzuri; haitokuwa rahisi lakini inawezekana na ili kujifunza mtu anatakiwa kuwa na nia na kuongeza jitihada ili kupata ujuzi na kuweza kuiongoza biashara katika muelekeo sahihi.