Home BIASHARA Vodacom yafungua fursa za kiuchumi mkoani Katavi

Vodacom yafungua fursa za kiuchumi mkoani Katavi

0 comment 159 views

Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Plc imeendelea kuwasogezea huduma wateja wake kwa kuzindua duka kubwa la kisasa katika wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi. Duka hili litawezesha kufungua fursa mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa wilaya hiyo na maeneo yanayoizunguka.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa duka hilo, Mgeni rasmi Waziri Mkuu Mstaafu Mh Mizengo Pinda, aliipongeza kampuni ya Vodacom huku akisisitiza kwamba duka hilo litarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja na kuchochea shughuli za kiuchumi za wilaya na mkoa huo.

“Karibuni nyumbani Vodacom, hongereni sana kwa kutufungulia duka kubwa zaidi hapa Mpanda kwani wilaya hii ina wananchi wachapakazi, wenye muamko wa kukuza uchumi na wafanyabiashara wakubwa na wadogo. Ni furaha kuona sasa watapata huduma za simu kwa ukaribu, lakini pia, wajasiriamali watapata fursa zaidi” alisema Mh Pinda huku akihamasisha wakazi wa wilaya hiyo kuona duka hilo kama kichocheo cha kukuza uchumi wilayani humo.

Duka hilo jipya Iina vifaa vya kisasa, wafanyakazi waliopata mafunzo sawia na walio tayari kutoa huduma bora kwa wakazi wa wilaya ya Mpanda kwa kuzingatia ongezeko la idadi ya watu katika mkoa wa Katavi.

Naye Mkuu wa mauzo wa Vodacom Kanda ya Nyanda za Juu kusini, MacFydine Minja alisema, uzinduzi wa duka hilo unaenda sambamba na mkakati wa kampuni hiyo wa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuleta fursa kwa watanzania. Pia Vodacom imelenga kupanua wigo wa huduma za simu Tanzania na kuzifikisha karibu na wananchi.

“Tumejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja wetu katika mkoa huu, ambapo tayari tuna huduma ya 4G ambayo inatoa nafasi ya kupata intaneti yenye kasi zaidi, pia tuna madawati matano ya huduma kwa wateja. Kipaumbele chetu ni kuhakikisha kwamba wateja wetu wanapata huduma kiurahisi na kwa ufanisi zaidi, hivyo uwepo wa Vodacom wilayani hapa ni fursa kwani duka na madawati ya huduma kwa Mteja tayari yameajiri wafanyakazi 15 na kutoa fursa lukuki za huduma mbalimbali katika duka hili kwa wajasiriamali mkoani hapa” aliongeza Minja.

Aliongeza kwamba kwa sasa wateja wa Vodacom wanaweza kupata huduma tofauti kwenye duka hilo kama vile usajili wa laini za simu, ushauri wa huduma za Vodacom kama M-Koba, kurudisha laini zilizopotea au kuharibika, kununua simujanja kwa bei nafuu kabisa na mengine mengi kutoka Vodacom.

Huduma za simu hasa miamala ya fedha imekuwa ikiongezeka kwa kasi nchini na kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla. “Nimekuwa nikipanga kuwa wakala wa M-Pesa kwa muda mrefu sana na sasa naishukuru Vodacom kwa kutufungulia duka hili, kwani leo naanza hatua ya kwanza ya kutimiza ndoto yangu” alisema Helena Lao, mkazi wa wilaya hiyo huku akionesha vitambulisho husika vitakavyomuwezesha kuwa wakala wa kwanza kusajiliwa katika duka hilo.

Kwa sasa Vodacom Tanzania Plc ina jumla ya maduka 100, madawati ya huduma kwa mteja (Service Desks) 350 yanayotoa huduma kwa wateja wa kampuni hiyo maeneo mbalimbali nchini.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter