Na Mwandishi wetu
Wachimbaji wadogo wa madini ya tanzanite yanayopatikana Mererani wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wameomba serikali kuunda chombo maalum ambacho kitanunua madini hayo moja kwa moja hapo Mererani, huku wakitaka yoyote atakayekutwa na madini hayo nje ya mji huo kushtakiwa kwa mujibu wa sheria kwa kosa la kuhujumu uchumi.
Mbali na kutuma maombi hayo kwa serikali, wachimbaji hao pia wameelekeza pongezi zao kwa Kamati ya Bunge ambayo wamedai imeeleza ukweli mzima wa mwenendo wa biashara hiyo ya madini, jambo ambalo limewagusa kwa kiasi kikubwa.
Wameomba serikali chini ya Rais John Pombe Magufuli kuhakikisha kuwa chombo hicho maalum kinaundwa haraka iwezekanavyo na wameshauri kisikose wafanyakazi ambao wana uelewa na wanafahamu thamani ya tanzanite ili waiwakilishe serikali vema pindi wanapofanya biashara.
Kamati zilizoundwa kuchunguza mwenendo wa biashara ya tanzanite na madini hapa nchini zilikabidhi ripoti zake wa Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai ambaye baadaye aliziwasilisha kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyezifikisha kwa Rais Magufuli jana Ikulu jijini Dar es salaam. Ripoti hizo zimeleeza kuwa ushauri mbovu na usimamizi dhaifu katika sekta hiyo umeisababishia nchi hasara ya mabilioni ya fedha.