Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa wananchi mkoani Kigoma kuchangamkia fursa za biashara zilizopo nchi jirani za Burundi na Rwanda ili kunufaika na biashara ya mipakani. Dk. Kijaji amesema hayo baada ya kukutana na kuzungumza na wafanyabiashara wa wilaya ya Kakonko kuhusu fursa na changamoto za kuendesha biashara katika eneo hilo.
“Nakuomba Mkuu wa Wilaya ya Kakonko uwakutanishe na kuwaunganisha wafanyabiashara hawa ambao nafurahi wengi wao ni vijana ili waandae andiko la namna ya kununua mashine za kuongeza thamani ya mazao ili wauze nje yakiwa yamechakatwa badala ya mfumo wa sasa ambao wanauza mazao ghafi, hivyo kupata hasara”. Ameeleza Dk. Kijaji.
Baadhi ya wafanyabiashara waliopata fursa ya kuzungumza na Naibu Waziri ambae alifika mahali hapo na Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Elijah Mwandumbya wameeleza kuhusu kushuka kwa bei ya mihogo na kudai kuwa hali hiyo inawaumiza wakulima kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake, Mwandumbya ametoa wito kwa wafanyabiashara kujenga tamaduni ya kulipa kodi kwa hiari ili kuisaidia serikali kupata fedha ambazo hutumika kuhudumia mahitaji muhimu ya jamii kama vile miundombinu, maji pamoja na afya. Kamishna huyo pia amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya kukusanya kodi na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili.