Na Mwandishi wetu
Kamishna wa kodi za ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ellijah Mwandumbya amesema kuwa, wafanyabiashara wanaotumia mashine za kielektroniki maarufu kama EFD’s kwa sasa ni zaidi ya 100,015. Kamishna huyo amesema hali hiyo inafanya serikali kukusanya mapato stahiki kulingana na biashara zinazofanywa.
Mwandumbya pia amesema serikali ilitoa zabuni za usambazaji wa mashine za EFD kwa makampuni tisa hivyo kuwezesha wafanyabiashara wengi zaidi kutumia mashine hizo kwakuwa zinapatikana kwa urahisi. Amezungumzia pia juu ya malalamiko ya wafanyabiashara ambao wanadai kulipa fedha lakini hawajapata mashine hadi sasa na kusema madai yao yanashughulikiwa.
Mbali na hayo, Kamishna huyo pia amesema serikali inafanya mchakato wa kufanya tathmini juu ya makampuni hayo ambayo yalipewa zabuni ili kutathmini utendaji wao wa kazi. Amefafanua kuwa tathmini hiyo itafanyika ndani ya mwezi mmoja na baada ya kukamilika, serikali kupitia mamlaka hiyo itatoa maamuzi yake.