Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira amesema serikali itawachukulia hatua wote waliohusika katika kuhujumu kiwanda cha kukoboa kahawa cha Tanganyika Coffee Curing Company Limited (TCCCO) na kukisababishia hasara ambayo imeacha kiwanda hicho na madeni makubwa.
Hadi kufikia Juni 30 mwaka huu, TCCCO ilikuwa na deni linalofikia Sh. 1,205,400,875.48 ambayo ni madai kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), manispaa, mishahara ya wafanyakazi, Astra Insurance, wastaafu, TCCCO saccoss pamoja na wadai wengine.
Baada ya kutembelea kiwanda hicho, Mghwira amesema serikali ya mkoa huo itaendelea kutafuta wale waliohusika katika kuiletea hasara kampuni hiyo akisema ni lazima majina yatajwe ili wajue wanamtafuta nani.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Japhet Ndosi ambaye hapo awali aliomba serikali kuingilia kati ili kukinusuru kiwanda hicho amesema hivi sasa baadhi ya wanahisa wamehama na kupeleka kahawa yao kukobolewa kwenye viwanda binafsi huku akitoa rai kwa serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutafuta wawekezaji wapya watakaokuwa tayari kuwekeza kiwandani hapo.