Wananchi wa kata ya Igamba wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe, wamejipatia ng’ombe wa maziwa 396 kutoka Shirika la Heifer International Tanzania ambalo pia limetoa msaada wa kiwanda cha kuchakata vyakula vya mifugo. Kupitia mradi wake wa maziwa shirika hilo limetoa ng’ombe hizo ili kuwasaidia wakazi hao kujiinua kiuchumi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika hilo, Rose Marando, amesema kuwa wanawapa wananchi ng’ombe jike ili pale zitakapozalishwa ngombe nyingine jike basi wale ambao hawakupata awamu ya kwanza nah ii ya pili waweze kupata.
“Kupitia kauli mbiu yetu ya ‘toa zawadi kwa mwingine kila aliyepewa zawadi awali anatakiwa na yeye atoe zawadi kwa mwingine ili kila mtu apate tunatamani huu utaratibu uende kizazi hadi kizazi na pengine wilaya nzima wapate ng’ombe” amesema Marando
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa kupitia ng’ombe hao wananchi watapata maziwa kwa ajili ya matumizi binafsi na kwa ajili ya kuyauza,pia watapata mbolea ambayo itatumika katika mashamba na hivyo kuleta maendeleo kwa wananchi hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Plingo, alipokua akikabidhi ng’ombe 75 wa awamu ya pili amewataka wananchi hao kuwapa matunzo stahiki ng’ombe hao na pale ng’ombe atakapokufa kwa uzembe basi mwananchi husika atalipia.