Home BIASHARA Wananchi waelimishwa kuhusu kodi

Wananchi waelimishwa kuhusu kodi

0 comment 106 views

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa elimu kwa wafanyabishara na wadau mbalimbali mkoani Geita juu ya masuala mbalimbali yanayohusu kodi, ikiwa ni pamoja na msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi.

Akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki Jukwa la Fursa za Biashara mkoani humo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa mamlaka hiyo Richard Kayombo amewataka wafanyabiashara wenye malimbikizo ya madeni ya kodi kupata msamaha wa riba na adhabu kwa asilimia 100 kupeleka maombi yao kwa kuwa zoezi hilo linachukua miezi sita pekee.

“Nachukua fursa hii kutoa wito kwa wafanyabiashara wote wenye malimbikizo ya madeni ya kodi na wote waliokuwa wakifanya biashara bila kusajiliwa kuwasilisha maombi yao TRA ili waweze kupata msamaha huu wa riba na adhabu wa asilimia 100 ambapo mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 30 Novemba, 2018″. Amesema Kayombo.

Aidha, Mkurugenzi huyo amewashauri wafanyabiashara wadogo waliopo kwenye utaratibu wa makadirio kusajiliwa na kupatiwa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) ambayo hutolewa na TRA bure bila ulazima wa kulipa kodi ya awamu ya kwanza kabla ya kuanza biashara isipokuwa ndani ya siku 90 baada ya kuanza biashara

“Awali wafanyabiashara walikuwa wanalipa kodi mara tu baada kusajili biashara zao na kukadiriwa kodi, lakini sasa hivi tumeweka utaratibu wa kulipa kodi ndani ya siku 90 kwa awamu ya kwanza baada ya kusajiliwa na na kuanza biashara” alifafanua Kayombo.

Aidha Kayombo amewataka wafanyabiashara na wadau mbalimbali walioshiriki jukwaa hilo la fursa za biashara kutoa risiti za kielektroniki za EFD kila wanapouza bidhaa, pamoja na kudai risiti pindi wanapopatiwa huduma au kununua bidhaa.

Vilevile, ameshauri wafanyabiashara wote walio na changamoto mbalimbali kuonana na Meneja wa TRA mkoani humo ili kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Jukwaa hilo la Fursa za Biashara limeandaliwa na Ofisi ya Mkoa wa Geita kwa kushirikiana na Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN) ambapo TRA imeshiriki jukwaa hilo kwa lengo la kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter