Na Mwandishi wetu
Baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga kutembelea kijiji cha Domanga na kufanya mazungumzo na warina asali, waokota matunda na wawindaji wa Kihadzabe, jamii hiyo imelalamikia juu ya kitendo cha wakulima na wafugaji kuharibu mazingira katika bonde la Yaeda Chini hivyo kuwakosesha asali na matunda.
Wakazi hao wamesema wanakabiliwa na hali ngumu kwa sasa baada ya uharibifu uliofanyika kutokana na vitendo vya ukulima na ufugaji. Wamedai hawana shughuli nyingine ya kujiingizia kipato zaidi ya kurina asali na kuokota matunda hivyo basi uharibifu huo wa mazingira unawaathiri sana kimaendeleo.
Mbali na hayo, jamii hiyo pia imeomba kushirikishwa katika maamuzi ya kata na wilaya ili wapate watetezi wao katika masuala tofauti yanayohusu jamii zao. Mofuga amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hudson Kamoga kupeleka wataalamu ili waweze kusimamia mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kulinda mazingira.
Aidha, wananchi katika jamii hiyo wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uwakilishi ili wapate viongozi wa kuwasimamia.