Home BIASHARA Watoroshaji madini waonywa

Watoroshaji madini waonywa

0 comment 107 views

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameonya kuwa yoyote atakayekamatwa akitorosha madini atachukuliwa hatua kali za kisheria. Majaliwa amesema hayo wakati akifungua soko la madini mkoani Geita ikiwa ni utekelezaji wa agizo alilotoa Rais Magufuli kwamba kila mkoa unapaswa kuanzisha masoko ya madini.

Uzinduzi wa soko hilo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Madini, Doto Biteko, Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila, wabunge wa mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, wakuu wa mikoa jirani pamoja na maafisa wa serikali.

Waziri Majaliwa amewataka viongozi wa serikali kusimamia soko hilo kwa uaminifu na uadilifu huku wakizingatia Sheria, Kanuni na miongozo iliyopo kwenye sekta ya madini, lengo likiwa ni kudhibiti utoroshwaji wa madini hasa dhahabu kwenda nje ya nchi.

“Wizara ya Madini ishirikiane na vyama na mashirikisho ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuandaa mpango kazi mahsusi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya soko hili ili lisigeuke kuwa kikwazo kipya kwa wachimbaji na wafanyabishara wa madini”. Amesema Majaliwa.

Pamoja na hayo, Majaliwa amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha soko hilo linalindwa muda wote huku miundombinu yake ikibaki salama.

“Mkuu wa mkoa na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, nawaagiza hakikisheni suala hili mnaliandalia utaratibu haraka iwezekanavyo”. Amesisitiza Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa mikoa yenye kiwango kikubwa cha uzalishaji madini kuanza mara moja mchakato wa kuanzisha masoko ili yaanze kufanya kazi kabla mwaka wa fedha 2018/2019 haujafika tamati.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter