Benki ya Dunia imeridhishwa na utekelezaji wa Programu ya Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma Mkoani Mara.
Hayo yamebainishwa na Bi. Gemma N. Todd, Mtaalam wa Elimu kutoka Benki ya Dunia katika ziara ya ufuatiliaji wa pamoja alipotembelea Shule ya Msingi Bukanga JWTZ, Kiara, na Mwisenga B zilizoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma Mkoani Mara.
Amesema wameridhika na utekelezaji wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) na maboresho yaliyofanyika katika ufundishaji na ujifunzaji wa Elimu ya Awali katika Halmashauri hiyo kwa kuwa zana bora zilizoandaliwa na walimu na wanafunzi wa Elimu ya Awali, Darasa la Kwanza na la Pili zimewawezesha wanafunzi kujifunza kwa ufanisi zaidi ikiwa ni miongoni mwa afua muhimu za Programu ya BOOST.
“Kwa kweli tunawapongeza sana Mkoa wa Mara, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Hili tuliloliona katika Shule za Msingi manispaa ya Musoma si jambo dogo na tukiendelea kutekeleza miradi namna hii tutafikia malengo tunayoyatarajia” amesema Gemma.
Naye Ally Swalehe, Mratibu wa Mradi wa BOOST kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 250.9 kupitia Programu ya BOOST kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu, programu ya shule salama, Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini, maboresho ya ufundishaji na ujifunzaji wa Elimu ya Awali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Amesema lengo la ziara hiyo ya pamoja kati ya Serikali na Benki ya Dunia ni kubaini kiwango kilichofikiwa katika utekelezaji wa malengo ya programu.
Aidha, Mratibu wa Programu ya BOOST kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia Lawrence Mselenga amesema,
“tumefika na tumeona madarasa haya ya Awali na Msingi yanazungumza, hata mwalimu asipokuwepo unaona kabisa mwanafunzi anaweza kujifunza mwenyewe. Kwahiyo, unaona kiwango cha utekelezaji kwa afua hizi katika halmashauri hii umefanyika vizuri”.
Kwa upande wake Adam Janga Mratibu wa Programu ya BOOST Mkoa wa Mara amesema wataendelea kusimamia MEWAKA ili kuhakikisha Malengo ya programu hiyo yanafikiwa.