Home Elimu Kukosa uadilifu, uzalendo kwatajwa tatizo kubwa kuliko kukosa elimu

Kukosa uadilifu, uzalendo kwatajwa tatizo kubwa kuliko kukosa elimu

0 comment 229 views

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba ameeleza kuwa kwa sasa kuna tatizo la uadilifu na kukosa uzalendo kuliko tatizo la kukosa elimu.

Gavana Tutuba ameyasema hayo mwishoni mwa mwiki jijini Mwanza wakati wa mahafali ya pili ya Chuo cha BoT.

Amewataka wahitimu wa Chuo cha BoT waliotunukiwa Stashahada ya Uendeshaji na Usimamizi wa Benki na Stashahada ya Uzamili katika Uongozi wa Benki kulitumikia taifa kwa uadilifu na uzalendo mkubwa.

“Wapo baadhi ya watu katika sekta ya fedha ambao wamekuwa wakifanya vitendo visivyo na weledi wala uadilifu na kusababisha hasara na kupungua kwa ufanisi wa sekta ya fedha, ikiwemo uwepo wa mikopo chechefu. Nawasihi sana msiwe miongoni mwa hao na badala yake muwe mfano wa kuigwa,” amesema.

Amesisitiza kuwa BoT inaendelea kuwafuatilia kwa karibu wafanyakazi wote wa sekta ya fedha na haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wale watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo visivyokubalika.

Aidha, amesema wahitimu hao wanajukumu la kuwa wabunifu, wachapakazi na kutumia ipasavyo ujuzi na elimu waliyoipata ili kuleta maendeleo kwao binafsi, jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla.

“Dunia ya sasa ni ya ushindani na inahitaji watu wenye ubunifu. Msipobuni namna za kutatua changamoto za watu wetu kwenye sekta ya fedha na kwingineko, elimu yenu inaweza isiwasaidie sana,” amesisitiza Gavana Tutuba.

Kwa upande wa elimu, Gavana Tutuba amewakumbusha wahitimu kuwa suala la kujiendeleza kitaaluma akisema ni muhimu kwa dunia ya sasa, kwani teknolojia na maarifa vinabadilika kila kukicha ambayo husababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya kiuchumi, kisayansi, ongezeko la watu na mabadiliko ya hali ya hewa.

Amesema “nawahimiza kuwa kuhitimu kwenu siku ya leo kuwe ni chachu na mwanzo wa safari mpya ya kujifunza na kupata maarifa mapya katika maeneo na viwango mbalimbali.”

Gavana Tutuba amekitaka Chuo hicho kutoa mafunzo na kufanya kazi zake katika viwango vya kimataifa ili kukifanya kuwa moja ya vyuo mahiri duniani na programu zake ziendane na mahitaji na mazingira ya sasa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter