Home BIASHARAUWEKEZAJI Korea Kusini yaahidi kuwekeza zaidi Tanzania

Korea Kusini yaahidi kuwekeza zaidi Tanzania

0 comment 196 views

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Biashara kutoka nchini Korea Kusini Ahn Dukgeun ambapo  ameeleza kuwa nchi hizo zitaendelea kudumisha ushirikiano uliopo katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma, Dkt. Biteko alimuhakikishia Dukgeun ushirikiano kutoka Serikali ya Tanzania katika kukuza uwekezaji na Korea Kusini hapa nchini.

“Niwahakikishie ushirikiano na utayari wa Serikali ya Tanzania katika kuendelea kufungua milango kwa wawekezaji kutoka Korea Kusini muda wowote kwani tayari mahusiano ya nchi zetu mbili yana mizizi iliyokomaa” amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake Waziri Dukgeun amesema kuwa, Korea Kusini itaendelea kuhimiza wawekezaji wengi kuja kuwekeza Tanzania huku akieleza kuwa, moja ya vivutio vikubwa vya uwekezaji Tanzania ni amani na utulivu uliopo ambao unatoa nafasi kwa Wananchi na wawekezaji kuelekeza nguvu na muda wao katika shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi.

“Tutaendelea kuhimiza wawekezaji zaidi kutoka Korea Kusini kuja kuwekeza Tanzania kwani mazingira ya uwekezaji hapa ni mazuri na hali ya utulivu na amani inavutia zaidi kuwekeza bila kuwa na mashaka,” ameeleza Waziri Dukgeun.

Katika kikao hicho, Waziri wa Biashara kutoka Korea Kusini aliambatana na Balozi wa Korea Kusini hapa nchini Kim Sunpyo, Makamu wa Rais wa Benki ya Exim Korea, Hon Soon-Young, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Umeme Korea Kusini, Shin Myung Jun na Wakurugenzi wengine kutoka Wizara ya Biashara Korea Kusini.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter