Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius K. Nyerere umeendelea kuongeza hamasa na ufaulu kwa wanafunzi wa kike nchini katika masomo ya Hisabati na Sayansi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano uliokutanisha wadau wa mfuko huo uliofanyika katika kumbi za mikutano za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam, Naibu Gavana, Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, amesema kuwa mpaka sasa mfuko huo umetoa udhamini kwa jumla ya wanafunzi wenye ufaulu wa juu 72, ambapo kati ya hao 50 ni wanawake na 22 ni wanaume.
“Mafanikio haya yanaendana na lengo la mfuko la kuongeza ufaulu wa wanafunzi hasa wa kike katika masomo ya Sayansi na Hisabati. Haya ni mafanikio makubwa ya mfuko katika kuleta usawa wa kijinsia katika maeneo hayo nchini,” amesema Dkt. Kayandabila.
Amesema walianza kutoa udhamini kwa wanafunzi sita na sasa wameongeza udhamii hadi wanafunzi kumi.
Ameeleza kuwa mpaka sasa wanafunzi walionufaika na mfuko huo ambao tayari wameingia kulitumikia taifa ni takribani 42.
Ameongeza kuwa mkutano huo unatoa fursa ya kujuana, kubadilishana uzoefu katika mambo mbalimbali na kupata ushauri toka uongozi wa mfuko na BoT. “Mkutano huu unatoa nafasi kwa wadau wa mfuko kujadiliana kwa pamoja jinsi ya kuongeza ushirikiano kati yao, mfuko na Benki kuu ya Tanzania kwa ujumla,” amesema.
Naye Mwakilishi wa Familia ya Mwl. Julius K. Nyerere katika Bodi ya Wadhamini ya mfuko huo, Madaraka Nyerere, amewaasa wanufaika kumuenzi Mwl. Nyerere kwa kutumia elimu waliyopata chini ya udhamini wa mfuko huo kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili jamii inayowazunguka.
“Katika sera za Mwl Nyerere kwenye upande wa elimu alisisitiza umuhimu wa serikali kusomesha raia wake ili kuwaanda na mazingira watakayokutana nayo wakimaliza elimu na kuandaa vijana kushika nafasi za uongozi ambazo zinashikwa na watu wazima,” amesema Madaraka.
Azzah Saleh ni mmoja wa wanufaika wa ufadhili huo ambapo amesema ni muhimu wanafunzi kujitahidi kupata matokeo mazuri ili waweze kupata ufadhili.
Mkutano huo umewakutanisha wadau wote muhimu wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, wakiwemo wajumbe ya Bodi ya Wadhamini wa Mfuko, Kamati na Wanufaika wa ufadhali wa mfuko ikiwemo wahitimu na wanoendelea na masomo ndani na nje ya nchi.
Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwl Nyerere ulianza kutoa ufadhali katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/14.