Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Jamhuri ya Korea imekubali kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasilino (Tehama) nchini Tanzania.
Majaliwa amesema lengo la chuo hicho ni kuwasaidia vijana kuendeleza ubunifu wao na kuonesha namna wanavyoweza kuunda vifaa mbalimbali.
Amesema hayo Oktoba 27, 2022 baada ya kumaliza mazungumzo ya kiserikali na Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Han Duck-Soo katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu uliopo Seoul.
“Kwa Tanzania hii itakuwa na manufaa makubwa kwa sababu sehemu kubwa ya Watanzania ni vajana kati ya umri wa miaka 15 hadi 40, hawa ni wengi sana, na mpango wa Rais wetu wa kuwapa shughuli ya kufanya ni kujifunza kuingia kwenye teknolojia kwa kujenga chuo hicho.
Serikali imeamua kujenga chuo hicho eneo la Nara jijini Dodoma, ambako tukishakamilisha vijana wa Kitanzania watapata fursa,” amesema.