Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetangaza fursa ya mafunzo ya kilimo biashara kwa vijana.
Mafunzo hayo ambayo ni awamu ya kwanza yanatarajiwa kufanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Bihawana mkoani Dodoma kuanzia Februari 15, 2023.
Katika mafunzo hayo wanufaika ambao ni vijana watapatiwa elimu ya kilimo biashara kwa muda wa miezi mitatu ambapo baada ya mafunzo wahitimu watakabidhiwa mashamba kwa ajili ya kilimo kulingana na taratibu na masharti yaliyowekwa na Wizara.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo inaeleza kuwa serikali kupitia wizara inatekeleza Programu ya Kuwezesha Ushiriki wa Vijana katika Kilimo Biashara (Building a Better Tomorrow Youth Initiative for Agribusiness (BBT-YIA).
Program hiyo inatarajia kuongeza ajira kwa vijana kufikia milioni tatu pamoja na kuiongeza ukuaji wa sekta ya kilimo kufikia hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 (Ajenda 10/30).
“Kupitia BBT, Wizara inaratibu uanzishwaji wa mashamba makubwa ya pamoja (Block Farms) kwa ajili ya vijana ambapo mradi huu unatekelezwa nchi nzima kwa vijana wote wenye sifa watapata fursa ya kufanya kilimo biashara katika mnyororo wa thamani,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa tayari Wizara imetambua mashamba yenye jumla ya ekari 162,492 katika Wilaya za Chunya (Mbeya), Bahi na Chamwino (Dodoma) Misenyi na Karagwe (Kagera) na Uvinza na Kasulu mkoani Kigoma.
Imetaja sifa za vijana watakaoomba kupata mafunzo kuwa ni pamoja na kuwa Mtanzania mwenye umri wa miaka 18-40 mwenye kupenda kufanya kilimo biashara uzoefu wa mwaka mmoja na awe anashiriki katika shughuli za kilimo.
Maombi yote yatumwe kuanzia Januari 10 hadi Januari 30.