Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, amesema kuwa serikali ipo mbioni kuanzisha bima ya mazao kwa wakulima ili kuwawezesha kupata fidia pale mazao yao yatakapoharibika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Waziri huyo ameeleza hayo wakati wa uzinduzi wa ushirikiano wa kati ya mradi wa USAID-NAFAKA na kampuni ya kimataifa ya uzalishaji na usambazaji mbegu na viuatilifu (Corteva). Hasunga amesema kuwa licha ya wakulima kufanya kilimo kwa juhudi na kutumia gharama nyingi, serikali imetilia maanani hasara wanazozipata kila mwaka kutokana na majanga kama mafuriko, ukame, na wadudu.
“Bima ya mazao itakuwa kifuta jasho kwa wakulima nchini, badala ya kulia watakapopata majanga ya kuharibiwa mazao yao, wao watacheka kwa sababu watalipwa fidia”. Amesema Hasunga.
Vilevile, Waziri huyo ameeleza kuwa kutokana na uhitaji mkubwa wa viuatilifu nyanda za juu kusini, serikali ipo katika hatua za mwisho za kujenga kiwanda cha viuatilifu mkoani Mbeya.
“Tanzania tunazalisha pembejeo kwa asilimia 10 tu na asilimia nyingine 60 tunategemea nje ya nchi, tunatumia gharama kubwa kuagiza pembejeo ndio maana tunaendelea kujenga na kuanzisha viwanda mbalimbali vya kuzalisha mbegu na viuatilifu ili wakulima wetu wazipate kwa wakati na gharama nafuu”. Ameongeza Waziri huyo.